Monday 24 June 2013

MBUNGE WA CCM AHOFIA TANZANIA KUWA NA RAIS "SHOGA"


http://www.ippmedia.com/media/picture/large/Ally-Kessy.jpgMBUNGE wa Nkasi Kaskazini, Ali Keissy (CCM), amesema kuwa bila Watanzania kuwa makini na sheria mpya ya ndoa ijayo, huenda nchi ikapata rais, wabunge na madiwani wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja (mashoga).

Keissy alitoa kauli hiyo wakati akichangia mada katika mkutano wa siku tatu wa Chama cha Wabunge cha Kupambana na Ukimwi (TAPAC) uliomalizika jana mjini Dodoma.

Mbunge huyo aliwaomba viongozi wa dini kukemea kwa nguvu vitendo hivyo, pia alipinga hatua ya wazazi kuwapeleka watoto wao wadogo shule za bweni akidai kuwa huko ndiko wanakojifunza vitendo hivyo.

“Mnashindwa kulea watoto wenu, mnawapeleka shule za bweni wakiwa na miaka mitatu ili walelewe kizungu. Huko watapakwa mafuta ya KY na wataingiliwa,” alisema.

Keissy alitolea mfano mkutano mmoja uliofanyika jijini Dar es Salaam kuwa uliwashirikisha mashoga 400, jambo alilodai ni ishara kwamba wanaojihusisha na vitendo hivyo wanaongezeka, na hivyo kuitaka serikali kuwapiga marufuku.

Hata hivyo, baada ya mbunge huyo kuhitimisha mchango wake, mmoja wa vijana wanaojihusisha na mapenzi hayo ya jinsia moja, Abdilah Ally ambaye alikuwa amealikwa na TAPAC, alitetea kuwa jamii inapaswa kukubali kwamba matendo hayo yanafanyika.

“Tunatambua kuwa sheria haziruhusu vitendo hivi, lakini vipo na vinafanyika na tunapata maambukizi kwa kiwango kikubwa. Tunachokitaka tusinyanyapaliwe na jamii, bali tupewe huduma ya afya ya kujikinga na maambukizi.

“Mathalani mimi hapa nina wapenzi wanaume watatu ambao nashiriki nao mapenzi, sasa kama nimeathirika ina maana wote wale nao wamethirika,” alisema.

Akifunga mkutano huo, Naibu Waziri wa Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu, aliwasihi wanasiasa wasiwabague makundi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya ushoga, usagaji na matumizi ya dawa za kulevya.

Alisema kuwa makundi hayo yanakabiliwa na janga la maambukizi makubwa ya virusi vya ukimwi, hivyo wanahitaji kusaidiwa kuondoka katika makundi hayo badala ya kuwahukumu.
Mwalimu alifafanua kuwa miongoni mwa washiriki wa mkutano huo kutoka katika makundi hayo, alikuwa mtumiaji wa dawa za kulevya, lakini baada ya kupata msaada wa kiafya ameachana na vitendo hivyo na sasa anaendelea vizuri chini ya uangalizi.

Mkutano huo uliratibiwa na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), kama wadau wakuu waliotoa mada mbalimbali kuhusu jinsi wanavyopambana kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi.

Katika hilo, Mwalimu alisema kuwa serikali dhamira yake ni kufikia maambukizi asilimia sifuri, hasa kwa kutoa msukumo mkubwa kwa makundi ya wanawake, vijana na watoto ambayo yana maambukizi zaidi.

Mbunge wa Chambani visiwani Zanzibar, Yusuf Salam Hussein (CUF), alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanikiwa kupunguza maambukizi hayo kwa wanandoa kutokana na sheria ya kuwataka wapime ukimwi kabla ya kufunga ndoa.
CHANZO: TANZANIA DAIMA

0 comments: