Tuesday 11 June 2013

AMRI KIEMBA ATUA YANGA, AKITOKEA SIMBA SC

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhEbK9s5RPR67iSlM-DV5ZYggxRTQq4LmWtJtZIQQUeDOECTko2vTTTS6OI-Jk4R5pQb5wqE8LjlAnIQgwjpy2XjwIkGYBBZ7urBrDPkNLMqdveegHE58aGMfPZJxBK0AtiOwFxZHgaoQg/s640/AMRIKIEMBASIMBA.jpg



  KOCHA Mkuu wa timu ya Simba, Abdallah Kibadeni, amebariki kuondoka kwa kiungo, Amri Kiemba, aliyejiunga na Yanga akiwasihi viongozi wa klabu hiyo wamwache akatafute masilahi zaidi kwa ajili ya maisha yake.

Kauli ya Kibaedeni, nyota wa zamani wa Majimaji ya Songea, Simba na Taifa Stars, imekuja baada ya kiungo huyo aliyeifungia Stars bao dhidi ya Morocco mwishoni mwa wiki ilipolala 2-1, kuripotiwa kuwa ametua Yanga kwa dau la shilingi mil. 35.

Kibadeni aliyejiunga na Simba siku chache zilizopita akitokea Kagera Sugar, alisema jana kuwa mpira ndio kazi ya kiungo huyo, hivyo kwa upande wake hatakuwa kikwazo na anamruhusu kwa mikono miwili kujiunga na Yanga kwa sababu anatafuta masilahi kwa ajili ya maisha yake.

“Kwa vile wachezaji wengi wa Tanzania soka ndiyo ajira yao, nashindwa kumzuia kwa vile kila mchezaji mwenye malengo amekuwa akipambana kufikia kiwango fulani katika maisha.

“Mimi inakuwa vigumu kumzuia Kiemba asiende Yanga kwa kuwa mpira ni kazi yake japokuwa ni pengo kubwa kwa Simba, namtakia kila la heri aweze kufanikiwa,” alisema Kibadeni.

Kibadeni alikwenda mbali zaidi na kusema kutokana na uwezo wa Kiemba dimbani, alitamani sana kuwa naye kwenye kikosi cha Simba, lakini imekuwa vigumu hivyo, anaomba Mungu apate mbadala atakaye fanya kazi kama kiungo huyo.

Kiemba ambaye ni miongoni mwa viungo mahiri wa sasa nchini, kabla ya kutua Simba aliwahi kuichezea Yanga kwa misimu kadhaa aliyokuwa amejiunga nayo akitokea Kagera Sugar ya Kagera, misimu kadhaa iliyopita.

Kiemba anakuwa mchezaji wa pili kutua Yanga akitokea Simba, amesaini mkataba wa miaka miwili huku kukiwa na habari kuwa atakuwa akilipwa mshahara wa sh milioni mbili kwa mwezi. Kabla ya Kiemba, Yanga ilifanikiwa kumsajili Mrisho Ngasa.

Alipotafutwa Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, kuhusu Kiemba, alisema anavyojua yeye ni kwamba mchezaji pekee kutoka Simba hadi sasa ni Ngasa na kama ni kweli wamemsajili Kiemba, watu wasubiri muda utakapofika.

0 comments: