Saturday 1 June 2013

KIGOGO WA CUF UTATANI KWA UCHOCHEZI VURUGU ZA MTWARA

Jeshi la Polisi nchini linadaiwa kumkamata Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa Chama cha CUF, Katani Ahmed Katani jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za uchochezi na kumsafirisha kwa ndege kwenda mkoani Mtwara.
Habari zilizolifikia Mwananchi Jumamosi na kuthibitishwa na Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro zilieleza kuwa Katani alikamatwa juzi mchana baada ya kupigiwa simu na maofisa wa polisi wa Kituo Kikuu cha Polisi jijini humo.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alipoulizwa juu ya kukamatwa kwa kiongozi huyo alisema hana taarifa huku akiomba apewe muda ili aulize.
“Sina taarifa ngoja niulize”, alisema kwa kifupi na hata alipotafutwa baadaye hakupokea simu yake ya mkononi.
“Alipigiwa simu juzi na maofisa wa polisi na kuelezwa kuwa anahitajika kituoni hapo, lakini alipofika alikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi” zilieleza habari hizo na kuongeza;
“Alihojiwa kwa saa kadhaa na jana asubuhi alisafirishwa kwa ndege kupelekwa mkoani Mtwara. Walitaka kumsafirisha kwa basi lakini viongozi wa CUF walikataa jambo hilo, hivyo kulazimika kusafirishwa kwa ndege.”
Habari hizo zilifafanua kwamba kwamba sababu kubwa ya kukamatwa kwa Katani ni kuhusishwa na vurugu zilizotokea mkoani Mtwara kati ya wananchi wanaopinga mradi wa bomba la gesi kutoka mkoani humo kwenda Dar es Salaam dhidi ya polisi.
Kwa upande wake Mtatiro alisema kuwa CUF hivi sasa inajipanga kuweka mawakili kabambe kwa ajili ya kumtetea kiongozi huyo wa vijana wa chama hicho.
“Tulijua tu kuna kiongozi wa chama atakamatwa maana kwa muda mrefu Polisi wamekuwa wakisema kuwa watawakamata viongozi wa juu wa chama. Kwa sasa Katani yupo Mtwara na sababu ya kukamatwa kwake ni kutuhumiwa kuchochea vurugu za Mtwara” alisema Mtatiro.


kwa msaada wananchi gazeti juni 1

0 comments: