Monday, 2 December 2013

GODBLESS LEMA KUONGOZA MAANDAMANO KUPINGA ONGEZEKO BEI YA UMEME

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema),Godbless Lema

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ameionya Serikali kuwa endapo itang'ang'ania kupandisha bei ya umeme nchini kwa asilimia 68 atakuwa mstari wa mbele kuongoza maandamano kupinga ongezeko hilo.

Lema alitoa onyo hilo mwishoni mwa wiki iliyopita jijini  hapa wakati akihutubia mkutano wa hadhara aliouitisha kwa ajili ya kuzungumza na wananchi juu ya mpango wake huo.

 Alisema inasikitisha baadhi ya viongozi wenye dhamana, wanasema iwapo mwananchi atashindwa kutumia umeme anaruhusiwa kutumia kibatari.

"Hii lugha siyo ya kiongozi na inapaswa kupingwa na kila mtu, kwani hatuhitaji ongezeko la gharama za umeme, bali tunahitaji kupunguziwa," alisema Lema.


Pamoja na kutotaja jina la kiongozi huyo, wiki iliyopita Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema bei ya umeme lazima iongezeke na kama kuna wanaopinga basi watumie vibatari.


Kauli hiyo  aliitoa baada ya Shirika la Umeme Tanzania kueleza dhamira yake ya kupandisha bei hiyo kutokana na  gharama za uzalishaji wa umeme kuwa kubwa na kwamba linatafanya hivyo baada ya kupeleka mapendekezo yake  Mamlaka ya Usimamizi wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).


Alitoa mfano wa nchi jirani ya Kenya kuwa serikali ya nchi hiyo kwa kuszhurumia wananchi wake, imepunguza bei ya umeme kwa asilimia 12, jambo ambalo lingepaswa kuigwa na serikali ya Tanzania.


Kwa upande mwingine, aliwaomba wafanyabiashara wasikubali kununua mashine za kielektroniki kwa ajili ya kukusanya kodi za biashara kama wanavyoamriwa na  Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambazo mikoa mingine wamekata.


"Nawaagiza mimi kama Mbunge wenu, msikubali kununua mashine hizi, sababu hii ni dili, ukitafuta katika mitandao unakuta zinauzwa Sh.50,000 hadi 100,000 , lakini TRA wanazuza kuanzia Sh. 600,000 na kuendelea," alidai Lema.


Lema alisema kuwa yeye siyo kama anapenda maandamano, lakini analazimika kufanya hivyo pale inapobidi kutafuta haki.

 
SOURCE: NIPASHE
2nd December 2013

0 comments: