Tuesday, 2 July 2013

USHURU WAWALIZA WAKULIMA WA MPUNGA (MOROGORO)

 


WAKULIMA wa mpunga wilayani Kilombero, Morogoro wamesema licha ya serikali kuwapiga mabomu wakati wakidai kupunguziwa ushuru, imeendelea kutoza ushuru kwa zaidi ya asilimia 200.
Awali mpunga ulikuwa ukitozwa sh 1,000 kwa gunia la kilo 100 lakini kwa sasa ushuru umepanda hadi sh 5,000 kwa gunia hilo au asilimia tano ya bei iliyopo sokoni kwa gunia.


Wakizungumza kwenye mkutano wa wadau wa kilimo cha mpunga Kilombero ulioandaliwa na Taasisi ya Maendeleo Mijini na Vijijini (RUDI) kwa kushirikiana na Jukwaa la Kilimo (ANSAF), walisema ushuru mkubwa ni kikwazo kwa wakulima katika kujikwamua kiuchumi.

Ushuru unatozwa asilimia tano ya bei ya soko ambapo gunia la kilo 100 linatozwa ushuru wa sh 5,000 huku wilaya nyingine zikitoza sh 3,000 kwa gunia la uzito huo.
Masumbuko Francis, mkulima wa mpunga alisema wanakumbana na ushuru kwa zaidi ya mara tatu na kwamba walipigwa mabomu walipokuwa kwenye maandamano lakini halmashauri ya wilaya hiyo inaendelea kutoza ushuru mkubwa.
“Wanunuzi wanakimbilia wilaya nyingine zenye ushuru mdogo… lakini pia kushusha bei ya mpunga kwa kuwa wametozwa ushuru mkubwa na serikali ni kumuumiza mkulima.

Alisema madiwani wanashindwa kuwatetea wananchi na kuwaacha wakandamizwe na ushuru mkubwa.
Mwekahazina wa Halmashauri ya Kilombero, Mbwana Msangi, alisema licha ya ushuru mkubwa wanalazimika kufanya hivyo ili kupata fedha za kujiendesha.
Wadau na wakulima waliofika kwenye mkutano huo walipendekeza kushirikishwa kwa wakulima katika suala la ushuru na kuupunguza hadi asilimia tatu.

na Rodrick Mushi, Morogoro Tanzania daima

0 comments: