Wednesday, 31 July 2013

MTANZANIA ATIMULIWA KWA AIBU BIG BROTHER AFRIKA

 

Nando. 

MSHIRIKI machachari katika mashindano ya Big Brother The Chase, Amil Khan maarufu kama Nando, juzi Jumapili usiku alitimuliwa kwenye jumba hilo baada ya kuingia na mkasi chumbani alipogombana na Elikem wa Ghana hali iliyowafanya waandaaji kuingiwa hofu.


Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja Uhusiano wa Multichoice Tanzania, Barbara Kambogi alisema ofisi yake imepokea taarifa hizo na kwamba mwakilishi huyo wa Tanzania alivunja masharti ya mchezo huo kwa kuhatarisha uhai wa mshiriki mwenzake Elikem.

“Nando amekuwa na tabia ya kubeba vitu hatarishi mara kwa mara, waandaaji wa mashindano walituvumilia kwa mara ya kwanza alipokutwa na kisu kwenye sherehe ya Channel O mwezi uliopita, lakini baadaye amegombana na mwenzake anaahidi kumuua, ule mkasi aliobeba kwenda nao chumbani ni kithibitisho,” alisema Kambogi.


Kambogi alisema bado haijafahamika rasmi ni lini Nando atarejea nchini kwani kwa sasa lazima atafutiwe mwanasaikolojia ili aweze kurudishwa katika hali yake ya kawaida.


Kabla ya kugombana na Elikem, Ijumaa iliyopita, Nando amekuwa na tabia ya kubeba vitu vya hatari mfukoni akiwa kwenye sherehe mbalimbali zilizokuwa zikifanyika ndani ya jumba hilo.

Baada ya kukutwa na kisu mwezi uliopita kwenye sherehe ya Channel O, Biggie(kiongozi wa jumba) alimwita na kumpa onyo la kwanza, lililohusu ukiukwaji wa sheria za mashindano kwa kutembea na silaha.


 chanzo mwanasport
By HERIETH MAKWETTA  
  Jumanne,Julai30  2013

0 comments: