Saturday, 27 July 2013

AFISA FEKI WA NIDA AKAMATWA NA POLISI

 


JESHI la Polisi mkoani Dodoma, linamshikilia mwanamke mmoja kwa tuhuma za utapeli kwa kuwadanganya wanafunzi wa vyuo vikuu, kuwa atawapatia kazi Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, David Misime, alisema alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kwamba mtuhumiwa huyo alikuwa akitumia majina tofauti ambayo ni Mariam Tawakali na Monica Ngaso (28).

Alisema hadi sasa mwanamke huyo amewatapeli wahitimu wa vyuo vikuu 29 ambapo kila mmoja alikuwa akitoa kiasi cha sh milioni 2.9 kwa madai ya kuwapatia kazi ya kuandikisha wananchi katika zoezi la vitambulisho vya taifa.

“Mwanamke huyo alikamatwa Julai 25 mwaka huu katika mtaa wa Barabara ya Sita katika Maniaspaa ya Dodoma.
“Jeshi la Polisi lilipata taarifa toka kwa raia wema kuwa kuna mwanamke anajitambulisha kwa baadhi ya wananchi kwamba anafanya kazi katika Manispaa ya Dodoma na anajishughulisha na zoezi la NIDA la uandikishaji wa vitambulisho vya taifa,” alisema.

Misime alisema mtuhumiwa huyo aliwatangazia wananchi kwamba zoezi hilo kwa mkoa wa Dodoma litaanza Agosti 2013 na kwamba kila anayehitaji kazi hiyo awasilishe maombi kwake.

Alisema maombi hayo yalitakiwa kuambatanishwa na vyeti vya sekondari au chuo, picha na fedha tasilimu sh 110,000 kama kiingilio.
“Mtuhumiwa aliwaambia waombaji hao kwamba ambaye angepata nafasi ya kufanya kazi angelipwa sh 400,000 kwa mwezi kwa kipindi cha miezi mitatu ambapo kazi hiyo ingekuwa imekamilika,” alisema.

Misime alisema mtuhumiwa alikamatwa na vyeti 29 vingi vikiwa ni vya wanafunzi waliohitimu vyuo vikuu mwaka huu.
Alitoa tahadhari kwa wananchi kuwa makini na watu wanaofanya vitendo hivyo. Mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani. 


IMEANDIKWA  na Danson Kaijage, Dodoma tanzania daima

0 comments: