RPC, RCO WAGEUKANA
KUNDI la
polisi wenye silaha za moto jana usiku walivamia nyumbani kwa Mwenyekiti
wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe,
kwa nia ya kumkamata.
Askari hao
wanaokisiwa kufikia saba, wakiwa na silaha nzito katika gari la wazi
waliwasili nyumbani kwa Mbowe majira ya saa saba na nusu usiku na
kuwaamuru askari wanaolinda nyumbani kwake kumtoa Mbowe nje ili waonane
naye.
Walinzi wa
Mbowe walihoji uhalali wa ukamataji huo na kuwataka polisi wawaoneshe
hati ya kumkamata, lakini hawakuweza kuionesha, hali iliyozusha wasiwasi
kwa walinzi wa kiongozi huyo.
Hata hivyo
walinzi hao waliwaambia polisi hao kuwa Mbowe ambaye pia ni kiongozi
mkuu wa kambi ya upinzani bungeni alikuwa safarini, jibu ambalo
lilipokewa kwa shingo upande na askari hao.
Polisi hao
baada ya kuona wameshindwa kukamilisha kazi hiyo, waliwaachia walinzi
hao namba ya simu 0754-085600 ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kipolisi
wa Kinondoni, Ernest Kimola, wakiwaagiza kuhakikisha wanamwambia Mbowe
awasiliane na kamanda huyo.
RCO amsukumia RPC, akana
Hata hivyo,
alipohojiwa na Tanzania Daima Jumapili kwa njia ya simu, Mkuu wa
Upelelezi Kimola aligoma kuzunguzia suala hilo na kumtaka mwandishi
kuwasiliana na mkuu wake wa kazi, ambaye ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kinondoni, Kamilius Wambura, akidai ndiye mwenye haki ya kutoa ufafanuzi
wa jambo hilo.
“Unajua mimi
si msemaji wa polisi, wasiliana na kamanda wa mkoa, maana ndiye mwenye
uwezo wa kutoa maelezo,” alisema Kimola na kukata simu. Lakini
alipopigiwa simu Kamanda Wambura aliruka kimanga, kwa mshangao, akidai
kutojua lolote kuhusiana na polisi kuvamia nyumbani kwa Mbowe.
“Kwa kweli
ndiyo napata taarifa hizo kutoka kwako, kuwa kiongozi huyo alifuatwa na
polisi, maana silijui suala hilo hata kidogo,” alisema Wambura, naye
kama alivyofanya Kimola akakata simu.
Kauli ya CHADEMA
Lakini
wakati Kimola akikataa kusema chochote, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk.
Willibrod Slaa, alisema kuwa alizungumza kwa njia ya simu na Kimola
kuhusiana na kitendo cha polisi kuvamia nyumbani kwa kiongozi huyo wa
juu wa kisiasa, na kudai kupewa majibu ya kushangaza.
Akizungumza
jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika Manzese, Wilaya ya Kinondoni,
Dk. Slaa alisema Kimola alijitetea akidai kwanza kukana kufika nyumbani
kwa Mbowe usiku wa manane. Pili, alisema kuwa hawakwenda kumkamata
Mbowe, isipokuwa kufanya naye mazungumzo na kisha wangemwacha.
Slaa alisema
kitendo hicho kimewashitua na ni cha kinyama na kilichokiuka sheria za
nchi na haki za binadamu. Aliongeza kwamba, daima wamekuwa wakilishutumu
Jeshi la Polisi kwa kutumika vibaya kukandamiza wapinzani, lakini mara
zote CHADEMA kimepuuzwa na sasa jeshi hilo limeamua kuvamia makazi ya
viongozi wa kisiasa kwa madhumuni yasiyoeleweka.
Alisema
haijulikani nini kingetokea ikiwa Mbowe angekuwa ndani, ikiwa walinzi
wangeamua kugoma kumwachia kiongozi wao. “Tuna hofu kubwa na usalama
wetu, maana pale wangeweza kufanya lolote, hata kumuua na kisha kutoa
matamshi kuwa walikuwa wanajibishana kwa risasi, kama ambavyo imekuwa
jadi ya askari polisi kutoa taarifa za uongo na upotoshaji wanapoua
watu,” alisema Slaa.
Alisema
ikiwa polisi walikuwa na shida ya kweli, wangemwita kwa njia sahihi na
si kumvamia na kuingilia uhuru wake na wa familia yake kama wanakamata
gaidi ama jambazi hatari.
Dk. Slaa
alisema Mbowe anayo ofisi inayojulikana, na kama kweli hakukuwa na jambo
baya lililopangwa na polisi hao wasingeweza kufanya uhuni kama
walioufanya.
“Kama
wanaweza kuvamia nyumbani kwa kiongozi mkubwa kama Mbowe wakiwa na
silaha nzito, itakuwaje kwa viongozi wa kawaida na raia?” alihoji Slaa.
Kutokana na
tukio hilo la kuogofya, CHADEMA imemtaka Rais Jakaya Kikwete kuwaeleza
Watanzania maana ya matukio haya ambayo yamedhamiria kuleta vurugu kubwa
nchini. Kadhalika, wamemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said
Mwema, kuueleza umma kile kilichokusudiwa na askari wake kuvamia
nyumbani kwa Mbowe mithiri ya jambazi.
Itakumbukwa
pia kuwa hivi karibuni askari polisi wa Mkoa wa Arusha walivamia
nyumbani kwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, wakiwa na silaha
nzito na mbwa, na kumkamata, kisha kumtupa rumande kwa siku nzima.
Chanzo chadema blog.com
0 comments:
Post a Comment