WAZIRI wa Maji Prof.Jumanne Maghembe (Mb)amewataka maafisa wa  Mamlaka  za Mabonde za  maji safi na usafi wa Mazingira Nchini kuacha urasimu wa utoaji wa vibali vya utumiaji wa maji na utupaji  maji taka kwa wananchi  na watu binafsi kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo.

Amesema kuwa watu wamekuwa wakiomba vibali hivyo kwa  muda mrefu lakini wamekuwa hawapewi kwa wakati ambao unatakiwa na muda mwingine hawapewi kabisa.

Prof.Maghembe  aliyasema hayo jana wakati wa ufunguzi wa mkutano  wa tano wa mwaka wa bodi za maji za mabonde ambao unafanyika katika hoteli ya  mtenda sun set uliopo Mkoani Mbeya.

“Mpaka kufikia septemba mwaka huu  nataka watu wote  yakiwemo mashirika yalioomba vibali hivyo vya maji  wawe wamepewa  na kama hawatakuwa wamepewa nimepewe ripoti kamili kujua tatizo  gani ambalo linakwamisha”alisema Waziri Maghembe.

Hata hivyo Prof. Maghembe alisema kuwa katika mkutano wa mwaka jana walibaini kuwepo kwa kasi ndogo ya utoaji wa vibali vya kutumia maji na kwamba zoezi hilo haliendani samba samba na mahitaji ya uwekezaji  nchini na kulingana na maombi yanayopokelewa katika ofisi za maji za mabonde.

Aidha  Waziri Maghembe alizitaka bodi za maji za mabonde kuendeleza juhudi za utoaji wa  vibali kwa wakati kwa kuzingatia utaratibu uliopo.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu  wizara ya maji  Mhandisi ,Bashir Mrindoko alisema kuwa  ofisi za mabonde  zimeendelea  na uandikishwaji  wa  watumia maji, pamoja na utoaji wa vibali  vya kutumia maji  na ukusanyaji wa maduhuli  kwa mujibu wa sheria ya rasilimali za maji.

Aidha Mhandisi Mrindoko aliwataka  maafisa wa mabonde  kuacha tabia ya kufanya kazi kwa mazoea  katika maeneo yao ya kazi ambayo wanafanyia.

‘Kitendo cha kufanya kazi kwa mazoea kinafanya hata utendaji kuwa mbovu miongoni mwetu kutokana na tabia tuliyojijengea hivyo ndugu zangu tubadilike ili tuweze kusonga mbele”alisema.
Mwisho.