SERIKALI imewataka wazazi kuhakikisha wanafunzi wote 36,000
waliofeli kidato cha pili mwaka jana na kutakiwa kurudia darasa hilo
wanafanya hivyo vinginevyo hawataruhusiwa kufanya mtihani wa kidato nne
mwakani.
Tahadhari hiyo ilitolewa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, wakati akifungua mafunzo ya Waratibu
Elimu kata Kitaifa yaliyoendeshwa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa
Elimu (ADEM) wilayani Bagamoyo, Pwani.
Mulugo alisema kuna taarifa ya kuwepo kwa baadhi ya wanafunzi hao
kushawishiwa na wakuu wa shule pamoja na wazazi wao kuendelea na kidato
cha tatu kwa matumaini ya kuwa watafanya mitihani ya kumaliza kidato cha
nne mwakani, jambo aliloeleza kuwa halitawezekana.
Aliwaagiza Waratibu Elimu Kata nchini kufanya utaratibu wa kufuatilia
mara moja wanafunzi wote wa kidao cha pili waliofeli kama wamekariri
darasa hilo kama ilivyoagizwa na wizara na endapo watawabaini waliokaidi
watoe taarifa mapema, ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Awali, Ofisa Taaluma wa Mkoa wa Dar es Salaam, Benadeta Thomas,
alisema mafunzo hayo yanaendeshwa katika mikoa 11 nchini na ni
utekelezaji wa mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari ngazi za kata
na kwamba mikoa inayohusika ni Dar es Salaam, Mbeya, Morogoro, Mtwara,
Kilimanjaro, Singida, Ruvuma, Arusha, Tabora, Mwanza na Tabora
na Julieth Mkireri, Bagamoyo TANZANIA DAIMA
|
0 comments:
Post a Comment