Tuesday, 23 July 2013

AUWAWA KWA TUHUMA ZA WIZI WA NG'OMBE

 

MWANAUME mmoja ameuawa na wananchi wenye hasira wilayani Tarime katika mkoa wa Mara, kwa tuhuma ya kuiba ng’ombe mmoja mwenye thamani ya shilingi laki tatu.

Kamanda wa polisi katika kanda maalumu ya Tarime na Rorya, kamishina msaidizi wa polisi, Bw. Justus Kamugisha, amemtaja mwanaume huyo kuwa ni John Mang’era Hirengo (38) mkazi wa kijiji cha Kwisarara wilayani Tarime.

Kamanda Kamugisha amesema kuwa tukio hilo limetokea juzi majira ya saa 6:00 usiku, katika kijiji cha Kwisarara wilayani humo na kwamba alituhumiwa kuiba ng’ombe mmoja mali ya Wakuru Chacha Mayombo mkazi wa kijiji hicho.

Amesema kuwa baada ya kuiba ng’ombe huyo wananchi wenye hasira walimfuatilia na kufanikiwa kumkamata akiwa na ng’ombe huyo na ndipo wakamshushia kipigo kikali kilichoondoa uhai wake.
Ameongeza kuwa marehemu mara kwa mara alikuwa akituhumiwa kuwa ni mwizi sugu wa mifugo katika eneo hilo.

Aidha, amesema kuwa kufuatia tukio hilo hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa kuhusiana na mauwaji hayo na polisi bado wanaendelea na upelelezi juu ya tukio hilo.
CHANZO MARAYETU BLOG

0 comments: