Aliyekuwa kiongozi wa Mungiki Maina Njenga kwenye picha ya awali. Picha/MAKTABA
MFUASI sugu wa kundi haramu la Mungiki alijiua kwa kujitia kitanzi usiku wa kuamkia Jumatano Katika Kaunti ya Murang’a baada ya kupata habari kuwa polisi walikuwa wakimwandama.
Bw Peter
Gitau wa miaka 23 kutoka kijiji cha Ngaiko anadaiwa kuwa alihofia
kukamatwa na kushtakiwa na sheria mpya za kupambana na makundi haramu
ambazo zingemwelekeza korokoroni kwa miaka 14 ama faini ya Shilingi
Milioni moja ama zote mbili.
Mwili wake ulipatikana na jamii yake ukiwa umening’inia nyumbani mwake na kamba shingoni.
Katika ujumbe
aliouacha, kijana huyo alimlaumu aliyekuwa mwenyekiti wa kundi hilo Bw
Maina Njenga kwa kuwapotosha vijana wajiunge na kundi hilo na kisha
akawasaliti kwa kuwatema ili ajiokoe yeye mwenyewe.
“Yeye
alitwambia tujiunge na kundi hilo ili tujitafutie riziki kutoka kwa
steji za matatu na pia kwa vituo vya biashara. Baada ya kumkusanyia
ushuru huo na kumtajirisha, alijiunga na serikali hiyo na kutuacha
mikononi mwa serikali tuuawe na wengine wafungwe,” ujumbe huo ukasema.
Kwa mujibu wa jamii yake iliyoongea na Taifa Leo
Bw Gitau alihofia kuwa hatima yake ingekuwa sheria hizo au kuuawa na
maafisa wa polisi ambao wanasaka wafuasi wa kundi hilo kote nchini
kufuatia tangazo rasmi la Inspekta Mkuu wa Polisi Bw David Kimaiyo.
Jamaa hao
walifichua kuwa Gitau aliacha ujumbe huo aliokuwa ameuandika kwa
karatasi akiaga jamii yake kwaheri huku akihimiza wafuasi wa kundi hilo
waliteme na watii sheria.
“Hatima yangu
ilikuwa tu kufungwa ama kuuawa na serikali. Na kwa vile mimi sitaki
kuwatwika wazazi wangu jukumu la kuuza shamba ili waninasue kutoka kwa
makali ya serikali, nimeonelea nijipumzishe kwa hiali,” ujumbe huo
ukaongeza.
Gitau
aliandika kuwa polisi wangemkamata kwanza wangemuitisha hongo ya Sh100,
000 ili asiuawe ama kushtakiwa lakini baadaye wamwandame na kisha
kumuua.
Kero
Akithibitisha
kisa hicho, Afisa Mkuu wa Polisi katika Wilaya ya Kigumo Bw John Katumo
alisema Bw Gitau alikuwa kero kwa maafisa wa usalama kufuatia juhudi
zake za kukusanya ushuru haramu kutoka kwa sekta ya Matatu haswa katika
barabara ya Kaharate hadi Kangari.
“Tumekuwa tukimsaka lakini kwa bahati mbaya amejiua kabla ya tumpate.
Lakini nia
yetu haikuwa kumuua, tulikuwa tu tumuonye arekebishe mienendo yake ya
kuongoza vikundi vya kutoza magari ya uchukuzi na pia bodaboda ushuru
haramu,” akasema.
Alisema
amefurahia ujumbe ambao Gitau aliacha wa kuwahamasisha vijana watii
sheria ili kujiokoa wenyewe akisema kuwa wafuasi wa makundi yote haramu
hayana pa kujificha kwa sasa.
“Sheria
itawaandama kwani mienendo yao inaathiri pakubwa utangamano na maendeleo
katika jamii. Kazi yetu ni kuhakikisha maisha ya wananchi yanaendelea
kwa mkondo ulio sawa bila ya kutatizwa na vizuizi vya ujambazi,”
akasema.
SWAHILI HUB.COM
Na MWANGI MUIRURI
Imepakiwa - Wednesday, July 24
2013
0 comments:
Post a Comment