Monday, 22 July 2013

ONGEZEKO LA KODI 14% YA INTERNET :TISP YA SEMA NI MZIGO KWA MWANANCHI

CHAMA cha watoa huduma za mawasiliano ya kiintaneti Tanzania (TISPA) kimeilalamikia sheria mpya ya kodi na ushuru wa bidhaa hiyo iliyotangazwa hivi karibuni na serikali kwa kusema itachangia ongezeko la gharama za huduma hiyo kwa watumiaji wa kawaida.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa TISPA, Gregory Almeida, alisema kuongezeka kwa gharama hizo kutafanya jitihada za kufikisha huduma hiyo nchini kufifia.

Alisema hoja ya ongezeko hilo la asilimia 14.5 katika huduma za mtandao itakuwa ni moja ya sababu kuu katika kuongeza gharama za huduma ya intaneti kwa wananchi kwa kuwa kodi hii itapita moja kwa moja kutoka kwa watoaji huduma hiyo.

“TISPA inapenda kuharifu umma kwamba bei za huduma hii zitapanda kwa asilimia 14.5 zaidi ikiwa na ziada ya kodi ya mapato ya asilimia 18 ambayo atabebeshwa mtumiaji wa mwisho wa huduma. Hali hii inatokana na serikali kupandisha gharama,” alisema Almeida.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, walitarajia kabla ya kutangazwa kwa ongezeko hilo, serikali ingefanya mazungumzo na wadau kwa lengo la kupata mawazo yao kabla ya uamuzi iliouchukua.

Katibu wa TISPA, Frank Goyayi alisema ongezeko la kodi katika huduma hiyo itazorotesha wanachama wao katika kusambaza huduma hasa maeneo ya vijijini na hivyo kusababisha kurudi nyuma katika kufikia malengo ya milenia ya kupunguza umasikini kwa kutumia teknolojia ya intaneti.

---Hosea Joseph/TanzaniaDaima


0 comments: