MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa CCM, Sophia
Simba amesema anahofia CHADEMA wanaweza kunyakua Jimbo la Babati Mjini
au Vijijini.
Simba alisema CHADEMA inaweza kufanya hivyo iwapo viongozi na
wanachama wa CCM watabweteka na kutowahamasisha watu wengi kujiunga na
chama hicho tawala.
Kiongozi huyo alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na viongozi wa CCM
Mkoa wa Manyara kabla ya kuanza ziara yake ya siku tatu wilayani Babati.
Simba alisema viongozi na wanachama wa CHADEMA wanajituma katika
kufanya kazi zao kichama, hivyo ni vema CCM wakaacha mazoea ya
kuhamasisha kila chaguzi zinapokaribia.
“Mnawaona wenzetu wa CHADEMA wanavyohangaika huko kwa wananchi
kutafuta wapiga kura kwa nguvu, na hii inaleta wasiwasi kwamba ikifika
mwaka 2015 wanaweza hata kunyakua Jimbo hapa Babati, aidha Mjini au
Vijijini,” alisisitiza Mwenyekiti huyo.
Alisema ili kuifanya CCM iwe imara ni lazima viongozi wa jumuiya zote ikiwemo ya vijana kuhamasisha watu kujiunga.
Simba alisema uhamasishaji huo ikibidi uendane na wanachama hao kutotoa ada za uanachama ili kuwavutia wengi zaidi.
“Tafuteni wanachama kwa nguvu zenu zote, ikibidi hata msiwalazimishe
kulipa ada za chama na kuwaita wanachama wafu kwani mkiwaita wafu
wataenda kwa wenzetu wa CHADEMA wanakochukuliwa bure,” alisema Simba.
Alisema miongoni mwa sababu zilizokifanya chama hicho kishindwe kwenye
chaguzi ni kutowajibika ipasavyo katika uhamasishaji wa kutoa mwamko wa
kisiasa kwa wanachama wake.
Simba alisema hali ni tofauti kwa wapinzani wao ambao kila kukicha
wamekuwa wakihahangaika kwa wananchi huku wakifanya mikutano mbalimbali
ya kuwarubuni kisiasa.
Alisisitiza kuwa viongozi wasiwachukulie kimzaha mzaha wapinzani wao
kwani wanafanya mikakati na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
“Tuache kufanya kazi kwa mazoea, tunapofikiria sisi ni chama tawala na
kubweteka tukisubiri wakati wa kampeni tutaumia, wenzetu mnawaona,”
alisema.
na Mwandishi wetu, Babati Tanzania daima gazeti
0 comments:
Post a Comment