Monday, 15 July 2013

HAYA NDIO MATOKEO HALISI YA UCHAGUZI MDOGO WA KATA 26 KTK TRH 16/06 NA 14/07/2013 NCHINI SOMA HAPA

Yafuatayo ni matokeo ya Kata zote 26 katika chaguzi zilizofanyika tarehe 16/06/2013 na 14/07/2013
Ni matumaini yangu kuwa namba zinajieleza vizuri.

1. Asilimia ya Kura:
CCM wamepata 49%, Chadema 45%, CUF 5% vyama vingine 1%

2. Ushindi wa Jumla wa Kata:
CCM wameshinda kata 16 (moja wameshinda bila kupiga kura kwa kuwa hakukuwa na wagombea wa upinzani) na Chadema wameshinda kata 10.

3. MLINGANISHO NA HALI ILIVYOKUWA BAADA YA UCHAGUZI 2010
  • CHADEMA wameongeza viti 5
  • CCM wamepoteza viti 3
  • TLP na CUF wamepoteza kiti kimoja kimoja.

4. MAMBO YA KIMKAKATI YA KUZINGATIA KWA VYAMA HUSIKA

a. Vyama vya Upinzani.
Ukiangalia majimbo ya Stesheni (Nachingwea) na Mnima (Mtwara) wapanzani wakijumlisha kura zao walipata kura nyingi zaidi kuliko CCM, lakini CCM ameibuka mshindi. Hali hii ilikuwepo Kenye pia katika chaguzi mbili za kwanza za vyama vingi ambapo KANU ilikuwa inashinda, lakini kura za upinzani ni nyingi. Hapa ndipo inabidi kufikiria mkakati wa ushindi.

Niwakumbushe tu, wakati wa vita ya pili ya dunia Uingereza iliunda ushirika na Urusi, kwa kuwa waliona nguvu za Ujerumani wasingeziweza wakiwa wametengana. Japo kwa kweli hakukuwa na urafiki mwingine wowote wa dhati kati ya nchi hizi, lengo la ushindi kwa wote liliwaunganisha. Maadui huungana na kuwa rafiki wanapokuwa na tishio la pamoja. Vyama vya upinzani visipoona hivyo, CCM itaendelea kudumu miaka mingi sana ijayo, japo kwa kura kidogo zaidi na zaidi.

Wapinzani Tanzania kama wanahitaji ushindi, wanahitaji kufikiria hili. Ukiangalia jumla ya kura zilizopigwa, CCM wana 49% lakini wana viti vingi zaidi ya 50% vilivyogombaniwa. Hakika CUF ingeungwa mkono na CHADEMA NA NCCR Mageuzi Mtwara na Nachingwea CCM wangepoteza. Kadhalika CUF ingeunga mkono Chadema Kata ya Dalai Dodoma wangewashinda.

Hata hivyo kila chama kinapaswa binafsi kuendelea na kampeni za kujijenga kule ambako bado hawafahamiki, huku wakijitahidi kuhudumia vema wale waliowapa uwakilishi.

b. Chama cha Mapinduzi.
Kwa kweli chama chetu kikongwe Tanzania kinahitaji kujitafiti. Uchaguzi mdogo wa madiwani wa Oktoba 2012, CCM ilipoteza viti kadhaa. Kwa haraka haraka nakumbuka walipoteza Kata 4 zikiwemo ya Daraja Mbili Arusha, Kata ya Ipole wilayani Sikonge - Tabora, na kata ya Lengali wilayani Ludewa. Katika uchaguzi huu CCM wamepoteza kata 5 zilizokuwa mikononi mwao, na kupata mpya mbili zilizokuwa TLP na CUF.

Kipropaganda ni rahisi kuhesabu viti kuwa kati ya kata 26 mmeshinda kata 16. Kimoyomoyo mnajua kuwa mnawakilisha kata chache zaidi sasa kuliko awali. Ni vizuri kujiuliza kama chama iwapo mambo yako sawa ndani ya Chama. Je ni sera? Je ni watendaji? Je ni kubweteka? Je ni mbinu ambazo badala ya kujenga mvuto kwa watu zinazidi kuwafanya watu wakichoke na kukichukia chama hiki tawala? Je ni timu ya kampeni?

Kwa vyovyote vile ni lazima mfanye tafakari. Mfahamu pia kuwa mbinu za kutisha watu kwa vyombo vya dola na kufungua kesi za kubambikiziana, na kujaribu ku criminalize the opposition zinafanya wananchi wawachukie zaidi kuliko kuwapenda.

Hiyo ni tathmini yangu. Nakaribisha mjadala.

By Mtu wa shamba JamiiForums

 

0 comments: