Saturday, 20 July 2013

MFANYA BIASHARA WA KIGENI AKWEPA KULIPA KODI MIAKA 8

  RAIA wa kigeni, Henry Domzalski anayemiliki kampuni ya Beachfront ya jijini Dar es Salaam, anakabiliwa na tuhuma za kuinyima mapato serikali kutokana na kutolipa kodi, licha ya kuwa amekuwa akifanya biashara ya kupangisha nyumba kwa takribani miaka minane sasa.

Inaelezwa kuwa, raia huyo wa Australia na Marekani, anamiliki nyumba Msasani Beach, Kawe jijini Dar es Salaam ambayo kodi yake kwa mwaka sasa imefikia dola za Kimarekani 3,000 (Sh milioni 4.8) kwa mwezi, sawa na dola za Marekani 36,000 (Sh milioni 57.6) kwa mwaka. Kiasi hicho kinatajwa kupanda taratibu kutoka dola 15,000 (Sh milioni 24) kwa mwaka miaka ya nyuma.

Habari kutoka ndani ya kampuni hiyo zinasema kwa kipindi chote hicho, raia huyo wa kigeni amekuwa hatoi kodi hiyo serikalini akidai taasisi yake haifanyi biashara.

Taarifa za uhakika zinaonesha kuwa, tangu Februari 2006, kampuni yake ilikuwa imeipangisha
nyumba hiyo iliyo katika kiwanja namba 77 (Block No. 2) kwa kampuni nyingine iitwayo Maersk Shipping na Domzalski alikuwa akiwasiliana na mtu aitwaye Westerhof Ebbo kuhusiana na malipo ya pango la nyumba.

Kodi iliyokuwa ikilipwa na kampuni hiyo iliyopanga, ambayo ni ya raia wa Denmark ilikuwa kiasi cha dola za Marekani 2,800 (Sh milioni 4.48) kwa mwezi ambayo baadaye ilipanda hadi kufikia dola 3,000 (Sh milioni 4.8).

Baadhi ya nyaraka zilizopatikana zinaonesha kuwa Domzalski amekuwa akipokea fedha hizo kupitia akaunti yake ya Benki ya Hawaii nchini Marekani yenye namba 0003-071367. Aidha kumekuwa na mawasiliano ya mara kwa mara kati ya watu hao wawili kuhusiana na malipo hayo ya pango, kitu ambacho kinadhihirisha kuwa raia huyo wa kigeni aliamua kuidanganya serikali. Nyaraka zinaonesha kuwa kuanzia Machi 2011 kodi hiyo ilipanda hadi kufikia 2,550 kwa mwezi kabla ya kupandisha tena kwa mara ya mwisho mwaka jana kufikia dola 2,750 kwa mwezi.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo aliliambia gazeti hili kuwa haelewi jambo lolote kuhusiana na suala hilo na kwamba ameshukuru kupokea taarifa hizo. “Nitakachofanya ni kuwasiliana na Meneja wetu wa mkoa wa Kinondoni ili aweze kulishughulikia suala hili. Kwa sasa siwezi kusema lolote hadi hapo litakapofanyiwa kazi,” alisema Kayombo. 
Akizungumzia tuhuma dhidi yake, awali Domzalski alikataa kampuni yake kufanya biashara yo yote kwa kipindi kirefu na kwamba suala la kodi linafanywa na mwanasheria wake. 


Lakini alipotajiwa jina la mpangaji wake alikiri kumfahamu Ebbo, lakini akidai hakuwa mpangaji wake kama yeye binafsi isipokuwa yeye aliipangisha nyumba hiyo kwa kampuni ya Maersk Shipping ambao kimsingi ndiyo waliopaswa kulipa kodi.

“Unaulizia kuhusu kodi ipi? Kama ni TRA wanaopaswa kulipa siyo mimi, ni ile kampuni niliyoipangisha. Na huyo mtu sidhani kama ni raia wa Denmark, kwa ufahamu wangu alikuwa ni Mholanzi,” alisema Domzalski ambaye hata hivyo, hakutaka kusema kama nyumba hiyo bado imepangishwa kwa kampuni hiyo au la.


 chanzo  HabariLeo

0 comments: