Saturday, 6 July 2013

RAIS JAKAYA KIKWETE AWA MGENI RASMI NA REFARII KATIKA TAMASHA LA MATUMAINI J'PILI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Matumaini ambalo litafanyika kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mratibu wa tamasha hilo, Abdallah Mrisho, amesema Rais Kikwete amekubali kuwa mgeni rasmi ambapo atatoa neno la matumaini kwa maelfu ya watu wanaotatajiwa kujitokeza uwanjani hapo.

Mrisho alisema: “Rais Kikwete amekubali ombi letu la kuwa mgeni rasmi, atatumia nafasi hiyo kutoa
neno la matumaini kwa wote watakaojitokeza uwanjani hapo.

“Rais pia ndiye atakayefungua mechi ya Wabunge wa Simba dhidi ya Yanga ambayo inasubiriwa kwa hamu kubwa. Kama ujuavyo rais wetu ni mtu wa watu na ni mpenda michezo, hilo linajulikana siku zote.

Aidha, Mrisho ametaja shabaha ya tamasha hilo kuwa ni kuamsha upya imani ya Watanzania kwa nchi yao. Kuwafanya wawe wazalendo na kila mmoja kujiona analo jukumu la kufanya, kuhakikisha Tanzania yetu inapiga hatua.

“Mbali na Rais Kikwete, wengine watakaotoa neno la matumaini siku hiyo ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Global Publishers Ltd, Eric Shigongo.

“Wengine ni Mwenyekiti wa Taasisi ya East Africa Speakers Bureau Limited (EASB), Paul Mashauri, mwalimu wa kimataifa wa ujasiriamali, James Mwang’amba na mwanamitindo, Jokate Mwegelo.

“Wote hao, kila mmoja atakuwa na fursa ya kufikisha Neno la Matumaini ili kila atakayehudhuria Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, aondoke akiwa mpya, akiwa na matumaini mapya kwa taifa lake na maisha yake kwa jumla,” alisema Mrisho.

 

Source: GLOBAL PUBLISHERS LIMITED

0 comments: