Friday, 19 July 2013

APIGWA TEKE MAHAKAMA KUU

 
Kethi Kilonzo
Bi Kethi Kilonzo akiwa nje ya mahakama Nairobi Julai 10, 2013. Picha/PAUL WAWERU 
Na MWANDISHI WETU
Imewekwa - Friday, July 19  2013 at  12:06
WAKILI Diana Kethi Kilonzo amefungiwa nje ya uchaguzi mdogo wa useneta Makueni baada ya madai yake dhidi ya IEBC kukataliwa na mahakama. Chama cha Wiper hata hivyo kimepewa fursa ya kuteua mgombea mwingine.
Majaji Mumbi Ngugi, Richard Mwongo na Weldon Korir walisema madai yake yote dhidi ya uamuzi wa tume hiyo wa kumzuia kuwania hayana msingi.
Jaji Mumbi Ngugi alisema: “Itakuwa ni kupuuzilia mbali tamanio la Wakenya kwenye Katiba kuhusu maadili ikiwa tutakubali Kethi anufaike kutokana na kosa (kwamba kuna wengine waliojisajili wakiwa hawana stakabadhi zinazohitajika).” Kethi alikuwa amesema alitumia nakala ya kitambulisho cha kitaifa na pasipoti ambayo ilikuwa imemaliza muda wake wa kutumika wakati wa kusajiliwa.
Majaji hao walisema kuwa ni wajibu pia wa mpiga kura kufuatilia maelezo ya usajili, hasa ikizingatiwa kwamba muda ulitolewa na tume.

Walisema kijikaratasi cha IEBC cha kuonyesha mtu alifika kusajiliwa si thibitisho la usajili.
Majaji pia walipuulizia madai ya Kethi kwamba alionewa wakati wa kujitetea hayana msingi. “Mawakili wake Julie Soweto na Haron Ndubi walipewa muda kuhoji mashahidi na hasa mkurugenzi wa usajili wa wapiga kura wa IEBC Immaculate Kasait,” alisema Jaji Ngugi.

Ushahidi

Kuhusu chama cha Wiper, Jaji Mwongo alisema “hakuna ushahidi kwamba chama cha Wiper kilijua kwamba Kethihakuwa amesajiliwa kuwa mpiga kura. Chama hicho kina haki ya kushiriki uchaguzi.”
Uchaguzi mdogo wa useneta wa Makueni ambao kwa sasa umepangiwa kufanyika Julai 26 ulitokana na kifo cha babake Kethi, Mutula Kilonzo Aprili 27. Awali ulikuwa umepangiwa kufanyika Julai 22.

chanzo swahilihub.com

0 comments: