Wiki iliyopita katika safu hii nilijadili suala la kuanzishwa kwa kodi za simu katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu.
Ni jambo linaloonekana kuichanganya Serikali hasa
baada ya malalamiko ya wananchi, maana kila kiongozi anasema lake.
Waziri wa Fedha anasema hivi, Rais anasema vile, Waziri Mkuu anasema
lake, chama tawala kinasema vile! Huu ni mwiba.
Siyo kwamba napinga kulipa kodi. Hapana. Hakuna Serikali kokote duniani isiyotoza kodi wananchi wake. Idadi ya watu katika nchi yoyote ni rasilimali ya maendeleo kwani kama watu hao watalipa kodi kikamilifu, basi Serikali itakuwa na fedha za kutosha katika maendeleo.
Tatizo linakuja pale walipa kodi wakubwa wanaposamehewa halafu wale wasionacho wanabambikwa kodi maradufu.
Hata hivyo, wakati Serikali inahimiza wananchi wa
chini kulipa kodi, hata kutoka kwenye chanzo ambacho si mapato kama
simu, kuna misamaha mingi ya kodi inayotolewa kwa walipa kodi wakubwa
hasa wawekezaji.
Kwa mfano katika sekta ya madini, Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC), inatoa misamaha lukuki ya kodi kama kivutio kwao.
Kulingana na cheti cha vivutio hivyo ni pamoja na
kufutwa kabisa kodi kwenye mafuta ya mitambo na magari (ikilinganishwa
na Sh200 kwa lita wanayolipa raia) kwa muda wote wa utafutaji madini na
mwaka mmoja wa kwanza wa uzalishaji ambapo watalipa asilimia tano tu.
Misamaha mingine ni kwenye mapato juu ya mtaji, msamaha wa kulipa VAT kwa kuagiza bidhaa nje ya nchi na hata ndani.
Vilevile kampuni hizo hulipia kodi ya stempu kwa asilimia 0.3 tu kinyume cha sheria inayoitaka kuwa asilimia nne.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) misamaha ya kodi iliyotolewa kwa kampuni za uchimbaji madini pekee kwa mwaka 2011 ilikuwa Sh109.885 billioni huku misamaha iliyotolewa na TIC ikifikia Sh239.667 billioni.
Hii ndiyo sababu ya umaskini kuendelea nchini licha ya kuwa rasilimali nyingi yakiwamo madini. Ndiyo maana hata mikataba ya madini inafanywa siri kubwa.
Huo ni mfano mmoja wapo. Ipo mianya mingi tu ya ukwepaji wa kodi. Siyo kwa bahati mbaya ila ni kwa makusudi. Mbali na misamaha, tumesikia mara kadhaa, baadhi ya viongozi wa Serikali wakificha mabilioni ya fedha nje ya nchi. Kwa mfano zile Sh300 bilioni zilizofichwa Uswizi zimeishia wapi? Afadhali tulifanikiwa walau kupata chenji ya rada kwa msaada wa Uingereza, lakini waliohusika na mchezo ule mbona hawaguswi?
Hayo yote bado ukamkamue mwananchi wa kawaida Sh1,000 ya simu kwa mwezi?
CHANZO mwananchi gazeti
Posted Jumatano,Julai31 2013 saa 12:42 PM
CHANZO mwananchi gazeti
Posted Jumatano,Julai31 2013 saa 12:42 PM
0 comments:
Post a Comment