WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, anatarajia kuwa mgeni rasmi katika
uzinduzi wa kampeni ya kuwapatia wananchi vyeti vya kuzaliwa kupitia
ofisi za kata wanazoishi badala ya ofisi za makatibu tawala wa wilaya.
Uzinduzi huo utafanyika katika viwanja vya CCM Ilomba, jijini Mbeya kesho.
Taarifa kutoka serikalini zinaeleza mpango huo utasimamiwa na Wakala
wa Vizazi na Vifo (Rita) ambao watasimamia shughuli hizo za usajili.
Kwa upande wa wilaya ya Mbeya Vijijini, Tanzania Daima ilizungumza na
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Utengule Usongwe, John Mwanampazi, aliyesema
wamepata mafunzo ya kuandaa vyeti hivyo ambavyo mwananchi atapata siku
hiyohiyo kwa sh 7,000.
“Ni kweli zoezi hili litazinduliwa Julai 23 ambapo wananchi
hawatalazimika kwenda ofisi za wilaya bali watakuja katika ofisi zetu za
kata na vituo vya afya na watapatiwa vyeti vyao siku hiyohiyo tofuti na
sasa,’’ alisema Mwanampazi.Alisema watoto wote wenye miaka mitano,
watapatiwa vyeti hivyo bure, lakini waliozidi watatoa sh 7,000 na
kutakiwa kuwa na viambatanisho kadhaa ikiwemo picha moja ndogo.
Alivitaja vitu ambavyo mtu aliyezidi miaka mitano atatakiwa kuwa navyo
ili kupata cheti cha kuzaliwa ni tangazo la kuzaliwa mtoto, kadi ya
kliniki ya mwombaji, hati ya kusafiria kutoka uhamiaji, cheti cha
ubatizo, cheti cha kumaliza shule ya msingi, cheti cha kumaliza kidato
cha nne au cha sita, kitambulisho cha kupiga kura au barua ya ofisa
mtendaji wa mtaa.
Alisema vyeti hivyo humsaidia mtoto kuandikishwa shule, kuzuia ajira
ya watoto na utumiaji wa watoto katika vita, kuwawezesha wanafunzi
kujiunga na vyuo na elimu za juu na kupata mikopo ya elimu ya juu.
“Faida zingine ni lazima ili kupata ajira katika sekta za serikali,
majeshi ya ulinzi na usalama, ni kiambatanisho cha msingi ili kupata
kitambulisho cha taifa katika zoezi linaloendelea nchini na pia husaidia
kupata hati ya kusafiria (passport),’’ alisema Mwanampazi.
na Gordon Kalulunga Tanzania daima gazeti
|
0 comments:
Post a Comment