Siku moja baada ya uongozi wa Yanga kugomea
mechi zake kuonyesha na kituo cha Azam TV, jana wachezaji wa klabu hiyo
wamelalamika kutopewa fedha za zawadi ya ubingwa.
Mabingwa hao mwanzoni mwa mwezi huu walikabidhiwa
Sh70 milioni ikiwa ni zawadi ya ubingwa, lakini mpaka sasa wachezaji
hao hawajalipwa kama walivyoahidiwa.
Wakizungumza na gazeti hilijana kwa sharti la kutotajwa majina yao wachezaji hao walidai wanashangazwa na ukimya uliotawala wa viongozi wao kuhusu haki yao.
“Tunafahamu tayari wadhamini Vodacom wamezitoa fedha hizo, na tulitegemea tungezipata kwa wakati kama zilivyotolewa kwa wakati, lakini inashangaza mpaka sasa ukimya umetawala na wala hatujaambiwa lolote kuhusiana na hilo,” alisema mmoja wa wachezaji hao.
Mwingine aliongeza kuwa kama kweli uongozi umeridhia kuwakabidhi fedha hizo ni vyema wakafanya kwa muda huu wakati wakijiandaa na msimu mpya wa ligi kwani kwa kutofanya hivyo kutachangia kupunguza morali yao na wengine kucheza chini ya kiwango.
“Inashangaza eti tuanze msimu mpya wakati hata fedha za ubingwa msimu uliopita hatukupewa hii ina maana gani kwetu? Ni vigumu wachezaji wakacheza kwa moyo wakati wanaona hawajatendewa haki, uongozi uliangalie jambo hili kwa mapana na kulifanyia kazi kwani sisi pia tuna familia zinatutegemea,” alisema mwingine.
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrance Mwalusako aiimbia Mwananchi kuwa ni kweli wachezaji hao hawajapewa fedha, lakini watalipwa kwa muda mwafaka.
“Kila kitu kina taratibu zake hatuwezi kupokea
fedha na kuwapa wachezaji, wavute subira hata sisi tunafahamu umuhimu wa
kuwapa haki yao, watafanyiwa sherehe na kukabidhiwa fedha hizo”
alisema.
Mbali ya fedha hizo pia wachezaji hao wanadai kutolipwa ahadi yao waliyopewa ya Sh100 mil kama wataifunga Simba na kutwaa ubingwa msimu uliopita. Hata hivyo habari ambazo Mwananchi imezipata zinasema moja wa kiongozi wa juu wa timu hiyo amechukua fedha zote za zawadi ya ubingwa kwa lengo la kufidia deni lake analoidai timu hiyo.
CHANZO
Na Jessca Nangawe, Mwananchi
Posted
Jumatano,Julai31
2013
0 comments:
Post a Comment