Friday, 19 July 2013

MGOMO WA WALIMU KENYA ULIVYOZIMWA NA KNUT KUKAA KIMYA

 

  Nyamira
Walimu katika kaunti ya Nyamira wakiandamana barabara ya Nyamira- Kisii Julai 2013. Picha/HENRY NYARORA 
Na BENJAMIN MUINDI
Imepakiwa - Friday, July 19  2013 at  10:25 

NJAMA kali iliyoundwa na maafisa wa ngazi za juu serikalini Jumatano iliwasukuma walimu kumaliza mgomo wao wa kitaifa uliokuwa umelemaza masomo katika shule za umma kote nchini kwa zaidi ya wiki tatu.
Na kwa mara ya kwanza, duru ziliambia Taifa Leo kwa kina viongozi wa Knut walivyosukumwa pembeni kiasi cha kulazimika kumaliza mgomo huo ghafla
Muda mfupi tu kabla ya kutangaza kufungwa kwa shule zote za msingi za umma saa kumi jioni Jumatano, Waziri wa Elimu Jacob Kaimenyi, alifanya kikao cha faragha na maafisa wakuu kutoka afisi yake pamoja na wengine kutoka Wizara ya Leba wakiongozwa na Waziri Kazungu Kambi.

Katika mkutano huo, walikubaliana kufunga shule zote za msingi za umma kwa muda usiojulikana ili kushinikiza walimu kumaliza mgomo wao kwa misingi kuwa kufunga taasisi hizo kulimaanisha walimu wangekosa mshahara kwa angalau miezi mitatu.
Mpango huu, duru zilisema, ulikuwa tayari umejadiliwa na Rais Uhuru Kenyatta, naibu wake William Ruto na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) kama hatua ya mwisho kabisa baada ya walimu kukaa ngumu na kukataa kumalizamgomo mnamo Jumapili kama ilivyotarajiwa.
Waliokuwepo katika mkutano huo ni makatibu Colleta Suda na Belio Kipsang, Kamishna wa Leba Sammy Nyambari na manaibu wakuu wa makatibu Isaiah Nyaribo na Eimerita Haoya.
Wengine ni wakurugenzi Margaret Thiong’o (Huduma za Uwandani) na Margaret Okemo (Elimu ya Kimsingi).


Sababu nyingine ya kuandaa kikao hicho ni hatua ya Jaji wa Mahakama ya Viwanda, Linet Ndolo, kusema angetoa uamuzi kuhusu mashtaka ya kudharau korti dhidi ya Mwenyekiti wa Knut, Wilson Sossion na Katibu Mkuu Mudzo Nzili.
Inasemekana kuwa Prof Kaimenyi na kikao chake walipata mwanya wa kufinya Knut kiasi cha kulazimika kufutilia mbali mgomo huo.
Mpango ulikuwa kutoa taarifa ya haraka kubatilisha agizo la kufunga shule baada ya maafisa wa Knut kumaliza mgomo, zilidokeza duru zinazofahamu yaliyojiri lakini hazikutaka kutajwa kwa sababu ya usiri wa mazungumzo hayo.
Mkutano na wanahabari uliokuwa umepangwa saa saba mchana katika jumba la Jogoo ulisongezwa hadi saa kumi jioni pale majadiliano yalifanyika kati ya mawaziri na afisi ya Naibu Rais.
Lakini maafisa wa Knut walipata fununu za njama hiyo na wakafululiza hadi kwa afisi ya Naibu Rais William Ruto Prof Kaimenyi alipokuwa akijitayarisha kutoa taarifa kwa vyombo vya habari.


Ni hili lililopelekea kusukumwa mbele kwa mkutano huo wa wanahabari kwa saa tatu.
Bw Sossion amekanusha matukio hayo akisema Ruto ndiye aliyewaita ofisini mwake ili kuzungumza nao, jambo ambalo ofisi hiyo imekanusha vikali. 

Maafisa hao wanane wa Knut walilazimika kusubiri kwa muda wa saa tatu katika sebule ya ofisi ya Ruto kwani alikuwa kazini nje katika Taasisi ya Ustawi wa Teknolojia mjini Athi River.
Maafisa wake ambao waliomba wasitambuliwe walisema hakuwa tayari kukutana na Sossion na kundi lake.  
Hata hivyo, hiyo yote ilikuwa sehemu ya njama ya kuwasukuma kona mbaya Knut ili waitikie wito wa kumaliza mgomo huo bila masharti.
Kisha Prof Kaimenyi, katika kikao na wanahabari kilichochukuwa chini ya dakika tano, aliagiza shule zote za msingi za umma zifungwe na kuwaingiza baridi zaidi maafisa wa Knut waliokuwa wakisubiri kwa hamu kuzungumza na Ruto.

Maazimio
Kufikia wakati huo, Sossion alikana kuwa walikuwa katika ofisi ya Ruto tulipompigia simu lakini baadaye alikubali kuwa walikuwa wameenda kuwasilisha maazimio ya Baraza Kuu la Kitaifa la Knut (NEC) kwa naibu rais.
Katika mkutano mfupi na Ruto, maafisa hao walitia saini mpango uliojumuisha walimu kurudi kazini. Bw Cleophas Tirop aliwakilisha TSC.


Ruto aliambia walimu: “Pesa mlizopewa na TSC za marupurupu ya usafiri haziwezi kuongezwa wala kupunguzwa… bajeti yetu imekabwa mno.”
Aliwaambia pia kuwa matakwa yao ya marupurupu ya nyumba na matibabu yatajadiliwa kupitia Tume ya Mishahara na Marupurupu, ingawa serikali ilidokeza kuwa itawajumuisha walimu katika mpango wa Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Matibabu (NHIF).
Maafisa hao wa Knut waliomba serikali iwaondelee wakuu wao wawili mashtaka ya kudharau korti kwani walikuwa hatarini ya kufungwa jela miezi sita ama wapigwe faini ya Sh20 milioni.
Ni baada ya hapo ambapo maafisa hao walifululiza hadi ofisi za Knut na kutangaza kumalizika kwa mgomo mbele ya wanachama 40 wa NEC ambao wamekuwa wakikutana tangu Jumamosi.
Lakini alipokuwa akitoa tangazo hilo, Sossion aliongeza: “Jamaa wa cheo cha chini ameamua binafsi kufunga shule lakini sisi tumeshauriana na ofisi ya sawa. Hivyo, ingawa wamefunga shule zetu, sasa twazifungua.”

Tamko liliwaloudhi maafisa fulani wa serikali kwani ilionekana ni kama kwamba Knut itasifiwa kwa kufungua shule hizo. “Hata tunapozungumza sasa, wakurugenzi fulani wa TSC wanaagiza shule zilizofunguliwa zifungwe,” akasema Sossion.
Hata hivyo, Prof Kaimenyi alisema bado hajasema ni lini shule zitafunguliwa na iwapo serikali itaongeza muhula wa sasa kufidia siku zilizopotea wakati wa mgomo.

CHANZO SWAHILI HUB.COM

0 comments: