Monday, 15 July 2013

TAMKO LA RAIS KIKWETE KUHUSU WANAJESHI WALIO KUFA HUKO DURFUR NCHINI SUDANI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tamko la Rais na Amiri Jeshi Mkuu kuhusu tukio la Darfur

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameshtushwa na kuhuzunishwa sana na tukio la kushambuliwa na kuuawa kwa vijana saba hodari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania waliokuwa wanalinda amani katika eneo la Darfur, Sudan.

Kwa hakika, Rais amesikitishwa sana na kitendo hicho ambako wanajeshi wengine 14 wa Tanzania wamejeruhiwa na waasi wa Sudan na ametuma salamu za rambirambi za moyoni mwake kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na kwa familia za wafiwa wote.

Aidha, Rais Kikwete anaungana na Watanzania wote na hasa maofisa na wapiganaji wa JWTZ na familia za wafiwa kuomboleza vifo vya vijana hao hodari wa Tanzania. Rais pia anaungana na Watanzania wote kuwaombea wale walioumia katika tukio hilo waweze kupona haraka na kuendelea na majukumu yao ya
ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa.

Katika salamu zake za rambirambi kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Adolf Mwamunynge na familia za wafiwa, Rais Kikwete na Amiri Jeshi Mkuu amesema:
“Sina maneno ya kutosha ya kuelezea mshtuko, huzuni na masikitiko yangu makubwa kufuatia vifo vya vijana wetu hao ambao wamepoteza maisha yao katika shughuli muhimu sana ya utekelezaji wa majukumu ya Umoja wa Mataifa ya kulinda na kuleta amani katika eneo la dunia ambako maelfu kwa maelfu ya watu wamepoteza maisha yao kwa kushambuliwa na waassi.”

Rais Kikwete ameongeza kumwambia Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na familia za wafiwa ”Napenda kwa niaba ya Watanzania wenzangu niwahakikishieni kwamba hakuna shaka kuwa vijana wetu hao tokea walipokwenda  Darfur Februari mwaka huu, na kwa hakika tokea Tanzania ilipoanza kuchangia walinzi katika eneo hilo mwaka 2007, wamefanya kazi nzuri sana, kazi iliyoongozwa na weledi wa hali ya juu na kazi ambayo imeiletea nchi yetu heshima kubwa. Tutaendelea kuwaenzi kwa kujivunia kazi yao.”

Amesisitiza Mheshimiwa Rais Kikwete: “Nakutumia wewe Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza vijana wetu hawa. Kupitia kwao, natuma salamu za rambirambi kwa maofisa wakuu na maofisa wadogo pamoja na wapigaji wote wa Jeshi letu kwa kupotelewa na wenzao. “

“Aidha, kupitia kwako, natuma salamu zangu kwa wanafamilia za waliopotelewa na wapenzi wao na ndugu zao katika tukio hilo. Wajulishe kuwa naungana nao katika kuomboleza. Wajue kuwa uchungu wao ni uchungu wangu pia na wa Watanzania wote na kuwa kwa pamoja tunamwomba Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu. Vile vile kwa pamoja tunamwomba Mwenyezi Mungu azilaze peponi roho za marehemu. Amina”.

Kwa walioumia, Rais Kikwete amemwambia Jenerali Mwamunyange: “Naungana pia na Watanzania wenzangu katika kuwapa pole nyingi walioumia katika tukio hilo tukiwaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone haraka na kuendelea na shughuli zao za ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa.”

Vijana hao waliopoteza maisha yao na walioumia, walikuwa sehemu ya askari 37 na ofisa mmoja ambao walikuwa wanasindikiza msafara wa waangalizi wa kijeshi katika Darfur kutoka eneo la Khorabeche kwenda Nyara waliposhambuliwa na waasi kiasi cha kilomita 20 kutoka Khorabeche saa tatu asubuhi jana, Jumamosi, Julai 13, 2013.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.

14 Julai, 2013
 

0 comments: