MSICHANA Atu Gabriel mwenye umri wa miaka 20, mwanafunzi wa Chuo cha
Eden Hill kilichopo Kwamfipa wilayani Kibaha mkoani Pwani, amekutwa
amekufa chumbani kwa mtu anayetajwa kuwa ni hawara yake, Hafidh
Mohammed.
Tukio hilo lilitokea April 26, mwaka huu na kukusanya umati huku
mwanaume aliyelala na binti huyo akitokomea kusikojulikana.Marehemu
anadaiwa kuwa mwenyeji wa Makambako mkoani Njombe.
Akizungumza na waandishi wetu juzi Kibaha, mama wa Hafidh ambaye pia
ni mjumbe wa eneo hilo, Zainabu Saidi alisema mwanaye alimweleza kutokea
kwa tukio hilo asubuhi kulipokucha na kabla ya hapo, hakuwa akifahamu
kama alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na msichana huyo kwa vile
aliyekuwa akimfahamu ni mwanamke mwingine ambaye alizaa naye.
Mimi kwa kweli sikuwa na taarifa yoyote juu ya uhusiano wao na huyu mwanafunzi, nimeletewa taarifa asubuhi na kijana wangu huku akionekana kuchanganyikiwa, nimejaribu kumsihi asikimbie lakini imeshindikana
alisema mama huyo.
Wanafunzi wa chuo hicho kinachofundisha masomo ya biashara na habari
ambao walikataa kutaja majina yao waliliambia gazeti hili kuwa, marehemu
Atu aliwaaga anakwenda jijini Dar es Salaam kumuuguza wifi yake
aliyelazwa katika Hospitali ya Amana, Aprili 23, mwaka huu.
Hata hivyo, walisema uondokaji wake uliwapa maswali mengi kwani
tofauti na walivyotegemea kuwa angebeba mfuko mkubwa wenye nguo za
kubadili, yeye aliondoka akiwa na mkoba wake wa mkononi pekee hali
iliyoonesha hakuwa akienda mbali.
Walisema siku tatu baadaye walipatwa na mshtuko mkubwa baada ya
mlinzi wa hosteli yao kuwaletea taarifa za kifo cha mwenzao kilichotokea
katika chumba cha mvulana huyo anayeishi jirani.
Majirani waliozungumza walisema kwao haikuwa mara ya
kwanza kumuona msichana huyo, kwani mara kwa mara alikuwa akifika pale
ingawa akishaingia ndani hakuwa akitoka nje.
Walisema mara zote hizo, mwanaume huyo mwenyeji ndiye alikuwa akitoka nje na kwenda kumnunulia chakula.
Jeshi la polisi liliwasili eneo la tukio na kuukuta mwili huo ukiwa
umelala kitandani ukiwa hauna jeraha, lakini pembeni yake kulikutwa
vidonge ambavyo havikufahamika ni vya aina gani ambavyo pia
vilichukuliwa pamoja na mkoba wake hadi kituonis.
Minong’ono kutoka kwa majirani kuhusiana na vidonge hivyo
ilitofautiana, baadhi yao walisema huenda vilitumika katika jaribio la
kutoa mimba, wengine walisema inawezekana msichana huyo alipata ugonjwa
wa ghafla usiku na mwanaume huyo alikwenda kumchukulia vidonge hivyo
ambavyo havikuweza kumsaidia marehemu kupata nafuu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, SACP Ulrrich Matei alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kusema juhudi za kumtafuta mwanaume huyo
zinaendelea huku madaktari nao wakiendelea na uchunguzi wao ili kubaini
chanzo cha kifo hicho.
0 comments:
Post a Comment