WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema bila uwekezaji nchi haiwezi kusonga mbele na akawataka watendaji serikalini kubadili mtazamowao kuhusiana na suala zima la uwekezaji.
Ametoa kauli hiyo jana usiku
(Jumanne, Aprili 29, 2014) wakati akizungumza na wafanyabiashara na
wajasiriamali mbalimbali wa hapa nchini kwenye hafla fupi ya uzinduzi wa
Taasisi ya Mkoba Private Equity Fund inayojishughulisha na utoaji
mitaji kwa wajasiriamali wadogo na wa kati.
“Bila uwekezaji tunajidanganya… ni ukweli usiopingika kwamba
uwekezaji mkubwa unatoka kwenye sekta binafsi, kwa hiyo watendaji wetu
serikalini wanapaswa kubadili mtazamo wanaposhughulikia masuala ya sekta
binafsi,” alisema.
Alisema watendaji serikalini
wanapaswa kubadili mitazamo yao hasa wanapokuwa wanawasiliana na watu wa
sekta binafsi kwa sababu kwa mfanyabiashara yeyote wakati ni mali.
“Tanzania imejipanga kuelekea
kuwa Taifa lenye uchumi wa kati, kama kweli tunataka kufika huko mapema
ni lazima tuwachukulie wadau wa sekta kwa mtazamo wa tofauti. Siyo
anakuja kutaka taarifa unaanza kumzungusha bila sababu, anataka kusajili
kampuni unamwambia unajua mafaili hayaonekani wakati hakuna cha mafaili
wala nini bali unatafuta mwanya wa kudai chochote,” alisema.
Akizungumzia kuhusu utoaji mikopo
kwa ajili ya mitaji ya kibiashara, Waziri Mkuu aliitaka Taasisi ya
Mkoba Equity Fund ihakikishe inajenga kwanza uwezo wa wahusika ili
waweze kuzalisha mali kama ilivyokusudiwa.
Akitoa mfano wake binafsi, Waziri
Mkuu alisema wakati anaanza biashara ya ufugaji nyuki miaka mitatu
iliyopita, hakuwahi kuandaa mchanganuo wowote (write-up) wala hakuwahi
kuandaa mpango wa biashara (business plan). Matokeo yake, alikuwa anatoa
tu fedha mfukoni na kununua vifaa kadri mahitaji yalivyokuwa
yakijitokeza, jambo ambalo alisema si sahihi.
“Ninawasihi sana viongozi wa
Mkoba Equity Fund wasitoe mikopo kwa watu wanaotaka kufanya biashara
kama nilivyoanza mimi. Wekezeni kwanza kwa kuwajengea uwezo
wajasiriamali watakaoomba fedha za mitaji kutoka kwenye taasisi hii,”
alisisitiza.
Akitoa ushauri kwa wajasiriamali
wadogo waliotoa shuhuda zao kuhusu changamoto walizokabiliana nazo
wakati wakianzisha biashara zao, Waziri Mkuu aliwataka wasirudi nyuma
wala wasikate tamaa. “Fursa ni nyingi sana na mnaweza kufanya mambo
mengi. Kitu cha msingi ni kuwa na nia thabiti (determination).
Wajasiriamali walitoa shuhuda zao
ni Mkurugenzi wa kampuni ya Montage, Bi. Teddy Mapunda; Mkurugenzi wa
kampuni ya Go-Financing, Bw. Geoffrey Ndossi, Mkurugenzi wa kampuni ya
SIGA Ltd, Bw. Marwa Busigara na Mkurugenzi wa kampuni ya WIA, Bw. Eric
Mwenda.
0 comments:
Post a Comment