Ligi
ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) msimu wa 2013/2014 itakayochezwa kwa mkondo mmoja
inaanza kutimua vumbi Mei 10 mwaka huu katika vituo vitatu vya timu tisa kila
kimoja.
Timu
itakayoongoza katika kila kituo cha ligi hiyo itakayomalizika Juni 2 mwaka huu ndiyo
itakayopata tiketi ya kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa msimu ujao wa
2014/2015. Vituo hivyo ni Mbeya, Morogoro na Shinyanga.
Kituo
cha Morogoro ambapo mechi zitachezwa Uwanja wa Jamhuri kitakuwa na timu za
Abajalo FC ya Dar es Salaam, African Sports (Tanga), Bulyanhulu FC (Shinyanga),
Kariakoo SC (Lindi), Kiluvya United (Pwani), Mji Mkuu FC (Dodoma) Mshikamano FC
(Dar es Salaam), Navy FC (Dar es Salaam) na Pachoto FC (Mtwara).
Uwanja
wa Sokoine ndiyo utakaotumika katika kituo cha Mbeya chenye timu za AFC ya
Arusha, Magereza FC (Iringa), Mpanda United SC (Katavi), Njombe Mji FC (Njombe),
Panone FC (Kilimanjaro), Tanzanite SC (Manyara), Town Small Boys (Ruvuma),
Ujenzi (Rukwa) na Volcano FC (Morogoro).
Timu
za Eleven Stars ya Kagera, Geita Veterans (Geita), JKT Rwamkoma FC (Mara), Mbao
FC (Mwanza), Milambo SC (Tabora), Mvuvumwa FC (Kigoma), Simiyu United (Simiyu),
Singida United (Singida) na Wenda FC (Mbeya) zitacheza katika kituo cha
Shinyanga kwenye Uwanja wa Kambarage.
Orodha
ya usajili wa wachezaji wa timu zote kwa ajili ya RCL imetumwa kwa vyama vya
mpira wa miguu vya mikoa na klabu zote za RCL, FDL na Ligi Kuu ya Vodacom (VPL)
kwa ajili ya kipindi cha pingamizi ambacho kinamalizika Mei 4 mwaka huu.
Hata
hivyo, katika usajili uliowasilishwa na baadhi ya klabu imebainika kuwa kuna
wachezaji walioshiriki VPL, FDL na wale U20 za VPL waliocheza ligi msimu wa
2013/2014.
Kiongozi
yeyote atakayebainika katika udanganyifu kwenye usajili huo, awe wa klabu au
chama cha mpira wa miguu cha mkoa atachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni
ikiwemo kufikishwa katika vyombo vya kimaadili vya TFF kwa hatua zaidi.
Ligi
ya Mabingwa haina mdhamini, hivyo timu shiriki zitajitegemea kwa kila kitu, na
zinakumbushwa kuwahi vituoni.
0 comments:
Post a Comment