Thursday, 24 April 2014

UNHWA YA KOREA KUSINI KUISAIDIA NIMR KATIKA UGUNDUZI WA DAWA KWA KUTUMIA MIMEA


           Na Father Kidevu Blog, Dar es Salaam
Taasisi ya taifa ya utafiti wa magonjwa ya binadamu Tanzania (NIMR), imesaini mkataba wa ushirikiano na kampuni ya UNHWA ya Jamhuri ya Korea ambapo kampuni hiyo itaisaidia NIMR teknolojia mpya ya kufanya ugunduzi wa dawa za binadamu kwa kutumia mimea.

Makubaliano hayo yamesainiwa jijini Dar es salaam pembezoni mwa kongamano la 28 la kisayansi la NIMR, ambapo mkurugenzi mkuu wa taasisi hiyo Dk. Mwele Malecela amesema hatua hiyo ni muhimu katika shughuli za utafiti wa afya nchini na maendeleo ya taasisi kwa ujumla.

Dk. Mwele amesema teknolojia hiyo itaongeza uwezo wa kiwanda cha taasisi cha kutengeneza dawa kwa kutumia mimea kilichopo eneo la Mabibo External jijini Dar es salaam na kwamba itawezesha taasisi kujikita zaidi katika utengenezaji wa dawa za saratani mbalimbali pamoja na za kusaidia udhibiti wa virusi vya ukimwi.

Kwa upande wake afisa mtendaji mkuu wa kampuni hiyo ya NHWA bw. YOUNG WOO JIN amesema kampuni yake imefikia hatua hiyo kutokana na mchango wa NIMR katika masuala ya tafiti na ugunduzi wa dawa ambapo ameahidi kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo katika kiteknolojia ili kuiongezea uwezo.

0 comments: