Wednesday, 30 April 2014

SEMINA YA WAANDISHI KUHUSU UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU YAFANYIKA ZANZIBAR

PICT2016
Na Miza Kona Maelezo Zanzibar
TATIZO la Wananchi  kujichukulia hatua mikononi mwao na matumizi ya nguvu zisizo za lazima kwa baadhi ya vyombo vya dola ni changamoto kubwa inayodhoofisha utekelezaji wa haki za binadamu.
Hayo yameelezwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria Zanzibar HarusiMiraji Mpatani kwenye  mafunzo ya Haki za Binadamu yaliyoandaliwa kwa ajili ya Waandishi wa habari katika  Ofisi ya Kituo hicho  Migombani Mjini Zanzibar.
Amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu kujichukulia sheria mikononi mwao  pale inapotokea tuhuma  inayopelekea kuwepo kwa uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu.
Amesema licha ya juhudi zinazochukuliwa katika kuhakikisha kuwa sheria ya haki za binadamu zinafikiwa kwa jamii,  bado matukio ya uvunjwaji na ukiukwaji  wa Haki za binadamu yanaendelea kutokea nchini.
“Watoto na walemavu wamekuwa ni wahanga wakubwa wa matukio ya unyanyasaji na udhalilishaji wa kingono, mbali na hali dhaifu ya kimaumbile waliyonayo bado jamii haijabadili mtazamo kuwa kundi hili linahitaji kulindwa kutokana na vitendo hivyo”, alifahamiisha Bi Harusi.
Aidha ameeleza kuwa waandishi wa habari wanawajibu katika kusimamia haki hizo kwa kutoa taaluma juu ya haki za binadamu kwa jamii wanayoifanyia kazi kwa kutumia vyema kalamu zao ili kujiepusha kuandika habari zinapelekea  uchochezi na kusababisha uvunjifu wa haki za binadamu.
Amewataka Waandishi kufuatilia bila ya woga matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu ili kuweza kuibua matukio mbali mbali ili  sheria iweze kuzifanyia kazi na kuondosha matatizo hayo.
Mada nane zinatarajiwa kujadiliwa katika mafunzo hayo zikiwemo Ufafanuzi wa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Haki za Binadamu na nafasi ya Waandishi wa habari katika kusimamia Haki za Binadamu, Utawala bora pamoja na Utawala wa Sheria.
Mafunzo hayo  ya siku mbili yametaarishwa na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar  na yanawashirikisha waandishi wa vyombo mbali mbali  vya Habari vya Serikali na biinafsi nchini.

0 comments: