Monday, 28 April 2014

VIAZI VITAMU NI MKOMBOZI WA KIUCHUMI KWA WAKULIMA

  pics mkulima-picha

VIJANA wa wilaya ya Ikungi mkoani Singida wamehimzwa kuondokana na uvivu na badala yake waelekeze nguvu zao katika kilimo cha kibiashara cha viazi vitamu ili waweze kujikomboa kiuchumi.
Changamoto hiyo imetolewa na mkulima na mfanyabiashara wa zao la viazi vitamu na mkazi wa kijiji cha Nkuninkana,Ibrahimu Kilu (34) wakati akizungumza na MOblog juu ya kilimo hicho cha viazi vitamu ambacho pia ni  zao la chakula.
Amesema kuwa zao la viazi vitamu ambalo miaka ya nyuma lilikuwa ni zao la ziada (halikupewa umuhimu unaostahili) hivi sasa zao hilo lina soko zuri ndani na nje ya nchi.
“Viazi vitamu kutoka wilaya yetu ya Ikungi vinakimbiliwa sana na wafanyabiashara kutoka mkoa wa Dodoma,Morogoro,Dar-es-salaam,Tanga na mikoa mingine nchini, pia kuna wafanyabiashara wanatoka Zambia na Comoro Kwa hali hiyo soko la zao hilo ni kubwa na linalipa vizuri”,alifafanua Ibrahimu.
Ibrahimu amesema toka aanze kulima zao hilo kibishara miaka mitano iliyopita limemwezesha kujenga nyumba bora na ya kisasa yenye choo ndani,amenunua pikipiki,anao mtaji wa kutosha na anasomesha watoto wake bila shida.
“Kilimo cha kibiashara cha viazi vitamu kina faida nyingi kinainua mhusika kiuchumi na pia uhakika wa kukabiliana na makali ya njaa unakuwepo.Mfano mzuri ni kwamba mimi msimu uliopita nililima uwele katika mashamba yangu yote na nilipata chakula cha kutosha kwa miaka miwili mfululizo”,amesema na kuongeza;
“Msimu huu,kwa sababu nina chakula cha kutosha mashamba yote nimelima viazi vitamu kwa lengo la kuboresha uchumi wa familia yangu matarajio ni kwamba natarajia kuingiza mapato ya zaidi ya shilingi milioni tatu”.
Akifafanua zaidi, Ibrahimu amesema faida ya kilimo cha viazi vitamu ni kwamba msimu huu nikilima mashamba yote  viazi zao hilo la viazi hurutubisha ardhi kwa kiwango kikubwa na hivyo msimu ujao atakapolima uwele atakuwa na uhakika wa kuvuna zaidi ya lengo.
Wakati huo huo, wakulima hao wamelalamikia tabia ya wafanyabiashara kuwalazimisha kujaza viazi vitamu kwenye magunia aina ya rumbesa ambayo yana uzito wa zaidi ya kilo 130 ambao kisheria haikubaliki.
Kwa upande wake Afisa Kilimo na Mifugo wilaya ya Ikungi,Ayubu Sengo  amesema wakulima wenyewe ndio wanaochangia biashara ya viazi vitamu ifanyike kwenye magunia ya rumbesa.
“Wakulima wetu kwanza ni watu wa ajabu kidogo na uvivu fulani upo ndani yao badala ya wao kuvuna viazi na kuvijaza kwenye gunia wao wanamwachia mnunuzi avivune kwa maana ya kuvichimba na kuvijaza kwenye magunia ya rumbesa na ndipo mkulima atalipwa kulingana na idadi ya magunia ya rumbesa”,alifafanua Sengo. 
Na Nathaniel Limu, Ikungi SINGIDA

0 comments: