Ufaransa yataka kuepusha kugawika kwa taifa la CAR
Rais wa Ufaransa Francois Hollande.
Rais wa Ufaransa ameiambia Jamhuri ya
Afrika ya Kati, wanajeshi wa Ufaransa walioko huko watafanyakazi
kuiepusha nchi hiyo isigawike, na kuwapokonya silaha wanamgambo na
makundi ya wahalifu wanaowapiga vita Waislamu.
Akiwasili mjini Bangui kutoka Nigeria,
alikohudhuria sherehe ya miaka 100 ya muungano wa nchi hiyo, Rais
Hollande alikutana na rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya kati
Catherine Samba-Panza na pia kuwahutubia wanajeshi wa Ufaransa. Hii ni
ziara ya pili ya Francois Hollande tangu mwezi Desemba mwaka jana na
inakuja wakati kukiwa na ongezeko la wanajeshi wa kulinda amani katika
Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Siku ya Jumanne bunge la Ufaransa
lilipiga kura kurefusha muda wa wanajeshi wa Ufaransa nchini humo, licha
ya Wafaransa wenyewe kutounga mkono ushirikishwaji wa wanajeshi wao
katika koloni lake hilo la zamani.
Wakati huo huo Umoja wa Mataifa
umesema watu milioni moja wameikimbia nchi hiyo tangu kuanza kwa ghasia
za kimadhehebu mwaka uliopita na kwamba watu wapatao milioni 1.3
wanahitaji msaada wa haraka wa chakula katika nchi hiyo ya Afrika.
Miezi minne iliopita, Ufaransa ilituma
wanajeshi wake ambao kwa sasa wamefikia takriban 2000 katika nchi hiyo
ilio na idadi kubwa ya Wakristo, na waasi wa Kiislamu wa kundi la Seleka
walichukua madaraka baada ya mapinduzi waliyofanya mwezi Machi mwaka
Jana, na wamekuwa wakisukumwa nyuma na wanamgambo wa kundi la
"anti-balaka."
Kando na kuwepo kwa wanajeshi wa
Ufaransa, Wanajeshi 6000 wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika (MISCA) pia
wapo nchini humo huku takriban wanajeshi 1000 wa Umoja wa Ulaya wakiwa
bado wanatarajiwa kuwasili Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Samba Panza atoa wito wa kuundwa kikosi cha kulinda amani cha U.N
Hata hivyo akizungumza mjini Geneva,
baada ya miezi miwili ya kusimamia shirika la Umoja wa Mataifa la ulinzi
wa Raia mjini Bangui, Philippe Leclerc, amesema bado nchi hiyo haina
wanajeshi wa kutosha wa kulinda amani.
Ulinzi mdogo ulililazimisha shirika hilo la Umoja wa Mataifa kuwahamisha baadhi ya raia.
Rais wa mpito Samba-Panza mara kwa
mara amekuwa akitoa wito wa kuundwa kwa kikosi cha kulinda amani cha
Umoja wa Mataifa nchini mwake. Katibu Mkuu wa Umoja huo Ban Ki-moon
anatarajiwa kutoa ripoti wiki ijayo, ya kuangalia uwezekano wa
kukibadilisha kikosi cha MISCA kuwa kikosi cha Umoja wa Mataifa.
Netsanet Belay, Mkurugenzi wa utafiti na utetezi wa shirika laAmnesty
International, amelitaka baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuridhia
hatua hiyo mara moja.
Kwa upande mwengine madaktari wasio
kuwa na mipaka (MSF) wamesema zaidi ya wakimbizi 8000 waliwasili kusini
mwa nchi jirani ya Chad tangu mwishoni mwa mwezi wa January.
Hata hivyo kundi la antibalaka
linasemekana linawafuata Waislamu kule wanakokwenda na kujaribu
kuwashambulia wakati wakijaribu kukimbia ghasia.
Chanzo, dw.de/swahili
0 comments:
Post a Comment