Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wakiingia bungeni mjini Dodoma jana kuhudhuria semina ya kuchangia taarifa ya Kamati ya Kumshauri Mwenyekiti wa Muda wa Bunge kuhusu Kanuni.
Dodoma. Hofu imetanda kuhusu uwezekano wa kuvunjika kwa Bunge Maalumu la Katiba, kutokana na hatua ya CCM kutumia wingi wao kutaka kupitisha utaratibu wa kupiga kura za wazi.
Baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo, wameshauri njia pekee ya kunusuru mchakato huo ni kwa CCM kukubali kukaa meza ya mazungumzo.
Wakati wajumbe hao wakitoa angalizo hilo, taarifa zilizopatikana jana mjini Dodoma zilisema CCM, wameitisha kikao cha dharura cha wajumbe wake wote leo saa 8:00 mchana kwa agenda ambayo bado ni siri.
Habari hizo zinadai kuwa wajumbe ambao ni Wabunge na Wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wametumiwa ujumbe mfupi wa simu (SMS) wakitakiwa kuhudhuria kikao hicho bila kukosa.
"Mambo muhimu yatajadiliwa, Mwenyekiti
wa Cocas (umoja wa wabunge) anasisitiza mhudhurie bila kukosa,
mahudhurio yatazingatiwa," unasomeka ujumbe huo ambao gazeti hili
limeuona.
Baadhi ya wabunge wa CCM hususan
wanaotoka Kanda ya Ziwa wanaounga mkono kura ya siri, walidai kuwa kikao
hicho huenda kina nia ya kuwatisha ili walegeze msimamo wao.
"CCM wanaogopa kura za siri kwa sababu
moja tu, wakiiruhusu watakuwa hawanacontrol (udhibiti) wa wajumbe
kutoka Zanzibar ambao wengi wanataka Serikali tatu," alidokeza mbunge
mmoja ambaye hata hivyo, hakutaka jina lake litajwe.
Mbunge huyo alisema kwa tathmini yake,
kama utaratibu wa kura za siri utapita, karibu asilimia 80 ya wajumbe
wote kutoka Zanzibar, watapiga kura ya kupitisha rasimu ya muundo wa
Serikali tatu.
"Kwa hiyo CCM haitaki kabisa utaratibu
wa kura za siri, wanataka kura za wazi ama kura ya dhahiri ili waweze
kuwa na udhibiti wa wajumbe ili tusitoke nje ya msimamo wao," alidai
mbunge huyo.
Hata hivyo, wakati CCM ikishikilia
msimamo wa kura za wazi katika kupitisha rasimu hiyo, wabunge wake wengi
wa Tanzania Bara na wale wa Zanzibar wanataka upigaji wa kura za siri.
Akizungumza na gazeti hili jana, James
Mbatia alitahadharisha kuwa msimamo wa CCM kulazimisha kura za wazi,
siyo kuwatendea haki Watanzania na huenda ikawa chanzo cha machafuko na
kukwama kupatikana Katiba Mpya.
"Kulazimisha matakwa ya CCM badala ya
wananchi itakuwa ni chanzo cha machafuko na Watanzania hatuko tayari kwa
machafuko wala kuona damu ya Mtanzania inamwagika," alisema Mbatia.
Mbatia aliongeza kusema; ni vizuri
hiyo Rasimu ya Katiba tuiboreshe, tupunguze mengine na CCM kama wana
hoja wazilete bungeni na ziwe hoja zenye mashiko siyo vitisho,
hatutavuka hapa."
Mbatia aliwataka baadhi ya viongozi wa
CCM kutokujifanya wanamfahamu sana Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere
kuliko anavyomfahamu Joseph Butiku na Joseph Warioba walioshiriki
kukusanya maoni ya Watanzania kwa ajili ya Katiba Mpya.
"Nyerere hakuwa na mawazo mgando,
alikuwa na fikra pevu zilizokuwa zinakwenda na wakati na ndiyo maana
alikubali mapendekezo ya Watanzania asilimia 20 waliotaka mfumo wa vyama
vingi," alisema.
Alisema kama kweli viongozi wa CCM
wana dhamira ya kweli na muundo wa Muungano, basi wafute kwanza
mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ili sasa wazungumze.
"Mabadiliko ya 10 ya Zanzibar
yalitamka kuwa Zanzibar ni nchi na ina mipaka yake na mwenye mamlaka ya
kuigawa Zanzibar ni Rais wa Zanzibar... hilo tu tayari walikuwa
wamevunja Katiba ya Muungano.
Mbatia alisema ibara ya 2(A), ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano, imeweka bayana kuwa pale Rais anapotaka
kuigawa Zanzibar, atashirikiana na Rais wa Tanzania Zanzibar.
"Kwa katiba hiyo, Rais wa Zanzibar
amepora ardhi ya JK (Rais Jakaya Kikwete) kwa hiyo walishavunja Muungano
kisheria... kwa maneno mengine mabadiliko hayo ni uhaini dhidi ya
Katiba ya Muungano."
Mbatia alisema katiba siku zote ni
tendo la maridhiano na kuitaka CCM kuingia katika maridhiano, kama kweli
ina nia thabiti ya kuwapatia Watanzania katiba badala ya kutumia wingi
wao kuififisha.
Mwenyekiti huyo alisema anawashangaa
CCM kwamba wao ndiyo walioanzisha mchakato wa katiba na kuunda tume,
mchakato ukaendeshwa na Serikali ya CCM halafu wanayakataa mapendekezo
yake.
Mbatia alisema tume tano zilizoundwa
kwa ajili ya suala moja tu la muundo wa Muungano, zilikuja na
mapendekezo ya Serikali tatu na kushangaa CCM sasa kuhoji uadilifu wa
Tume ya Jaji Warioba.
Tangu kuanza kwa Bunge Maalumu la
Katiba, bunge hilo limetumia takriban siku 16 sasa katika kutunga rasimu
za kanuni na kubwa linalobishaniwa ni utaratibu wa upigaji wa kura.
Mapendekezo ya awali ya Kanuni za
Uendeshaji wa bunge hilo, zilipendekeza upigaji kura uwe wa siri na hata
wajumbe walipochangia na CCM kung'ang'ania kura za wazi, bado kamati
ilikuja na pendekezo la kura za siri.
Hata hivyo wajumbe wengi wanaotoka CCM
walipinga kwa nguvu zote kura za siriwakitaka za wazi na suala hilo
kurudishwa kwenye kamati, lakini hadi juzi kamati ilishindwa kuafikiana.
Kutokana na suala la upigaji kura
kuonekana ni tata, kamati iliyoundwa kupitia kauni hizo, juzi iliamua
kurudisha suala hilo kwa Bunge la Katiba ili ilifanyie uamuzi.
Oluoch ataka hati ya Muungano ipelekwe mezani
Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba,
Ezekiah Oluoch, ameuchambua Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba na kutaja
kitendo cha wajumbe wa Bunge hilo kutokugawiwa hati ya Muungano kuwa
moja ya kasoro kubwa zinazoukabili.
Akizungumza katika mahojiano maalumu
na gazeti hili jana, Oluoch alihoji mantiki ya wajumbe wa Katiba
kujadili Muungano, wakati hawana hati ya Muungano iliyosainiwa na
waasisi wake; Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume.
"Mimi nililiona hilo mapema, nikaenda
kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji FrederickWerema, nikamuuliza kama
atagawa hati ya Muungano kwa wajumbe, lakini inaonekana hakuna mpango
huo. Sasa tunajadilije Muungano wakati hatujui msingi wake," alihoji.
Oluoch alisema nguzo ya Bunge la
Katiba ni Muungano na kwamba matunda yake yataonekana kama kumewekwa
mazingira mazuri ya kuujadili.
"Lakini utajadilije Muungano wakati
huna nakala ya article of Union (hati ya Muungano). Mimi nilidhani ili
kwenda vizuri wajumbe wapewe kwanza nakala ya hati hizo," alisema.
Wawakilishi Zanzibar washikana mashati
Mwinyi Sadallah anaripoti kutoka
Zanzibar kuwa wakati Bunge la Katiba linaanza kesho mjini Dodoma,
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) wamesema kuna waraka
bandia umesambazwa ukieleza Baraza hilo limeazimia kwa pamoja kutaka
mamlaka kamili ya mataifa ya Zanzibar na Tanganyika.
Waraka huo umesababisha mgogoro na
kutoelewana kwa wajumbe katika kamati ya uongozi chini ya Mwenyekiti
wake Spika Pandu Ameir Kificho na Katibu wa kamati hiyo Yahaya Khamis
Hamad, baada ya kujitokeza hadharani baadhi ya wajumbe wakisema waraka
huo umeghushiwa na hawautambui.
Akizungumza na Mwananchi Spika Pandu
Ameir Kificho hakukubali au kukataa kuwepo kwa waraka huo na badala yake
akasema atakuwa tayari kuutolea maelezo atakapofika ofisini kwake,
licha baadaye alipopigiwa simu na kupokea akasema tena kuwa atautolea
majibu alasiri, jana jioni.
"Sina la kusema kwa sasa, acha nifike
ofisini nitakueleza kuhusu jambo hilo...niache ndugu yangu nifike ofisni
kwangu kwanza. Tafahali niko njiani hivi sasa, siko tayari kuuzungumzia
waraka huo au mwingine...niache nitakwambia baadaye ," alisema Spika
Kificho ambaye ni Mwenyekiti wa muda wa Bunge la Katiba.
Hata hivyo, alipopigiwa simu Katibu wa
Baraza la Wawakilishi Zanzibar Yahya ili atoe maelezo ya kina kuhusu
waraka huo iwapo BLW Zanzibar lilitoa azimio lake na kuliwasilisha kwa
Mwenyekiti wa Tume ya Mabailiko ya Katiba Jaji Joseph Sinde Warioba
kutaka mfumo wa serikali tatu. Awali alikubali na kukana akisema
inawezekana si waraka huo anaouzungumzia ila BLW limependekeza
kupatikana kwa mamaka huru ya Tanganyika na Zanzibar.
"Hapana waraka wa Azimio la Baraza
kutaka mfumo wa serikali tatu siutambui.Lililofanyika ni kutaka mamlaka
huru za Tanganyika na Zanzibar, pia kuna mambo mengi humo, sitaki
unihukumu kwa waraka ambao sioni katika simu. Ingefaa niuone kwa macho
yangu kama ndiyo wenyewe au la," alisema Yahya.
Akiuzungumzia waraka huo, Mnadhimu
ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza hilo, Salmin Awah Salmin
(Magomeni), alisema waraka upo ila ni wa kughushiwa kwa sababu hakuna
kikao cha kamati ya uongozi kilichowahi kukaa na kutoa azimio la pamoja
juu ya aina gani ya Muungano unaotakiwa kuzingatiwa katika uundwaji wa
Katiba Mpya ya Tanzania.
Salmin alisema kuwa waraka huo
umeandikwa kwa niaba ya kamati ya uongozi ya Baraza la Wawakilishi
Zanzibar na una saini ya Spika wetu Kificho jambo ambalo alisema si la
kweli bali ni la upotoshaji mkubwa.
Alisema kumbukumbu zinaonyesha tangu
kuanza kwa mjadala wa mabadiliko ya katiba, BLW Zanzibar halijatoa
msimamo wa pamoja na kuzingatiwa, badala yake kila upande wa kisiasa na
kiitikadi umekuwa na maoni yake ikiwa ni pamoja na kambi ya upinzani
kutaka mfumo wa Serikali ya Muungano wa mkataba na chama tawala
kusimamia mfumo wa Serrikali mbili.
Mnadhimu huyo alisema baaada ya
kufuatilia kwa undani aligundua kuwa kuna watu watano ndiyo
waliojifungia na kuutengeneza waraka huo ukitumia jina la Kamati ya
Uongozi na kwa niaba ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuutayarisha na
kujenga hoja wanazozitaka wao kwa matakwa yao.
Chanzo, mwananchi
0 comments:
Post a Comment