Sunday, 3 August 2014

NOOIJ APANGUA KIKOSI STARS, NGASSA NA OSCAR JOSHUA WAPIGWA MKEKA, MOURAD NA MCHA WANAANZA LEO DHIDI YA MAMBAS

 

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mart Nooij amefanya mabadiliko madogo katika kikosi chake kitakachomenyana na Msumbiji, Mambas jioni ya leo Uwanja wa Zimpeto mjini hapa.
Nooij aliyewahi kuifundisha Msumbiji, atamuanzisha Khamis Mcha ‘Vialli’ badala ya Mrisho Ngassa na Said Mourad badala ya Oscar Joshua wakati, wengine wote ni wale walioanza mchezo wa Dar es Salaam.   
Mcha aliingia kumpokea Ngassa kipindi cha pili Dar es Salaam na akafunga mabao yote mawili katika sare ya 2-2 moja kwa penalti.
Tuko tayari; Kocha Mart Nooij akiwaongoza vijana wake kuingia Uwanja wa Zimopeto jana tayari kwa mazoezi ya mwisho kujiandaa na mchezo wa leo

Nooij ambaye amesema anakiamini kikosi chake kuelekea mechi ya marudiano ya hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Morocco, anahitaji ushindi wa ugenini ili kusonga mbele.
La kama si ushindi, basi sare ya kuanzia mabao 3-3, baada ya awali kulazimishwa sare ya 2-2 na Mambas Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam- na kama matokeo yatakuwa 2-2 tena, mchezo utahamia kwenye mikwaju penalti kuamua timu ya kwenda kwenye kundi lenye timu za Cape Verde, Niger na Zambia.
Akizungumza mjini hapa baada ya mazoezi ya jana jioni, Nooij ambaye ni raia wa Uholanzi alisema ana imani na timu yake itacheza vizuri zaidi kuliko Dar es Salaam kwa kuwa haitakuwa katika shinikizo la mashabiki kama nyumbani, ambalo maranyingi hufanya wachezaji wapoteze hali ya kujiamini.
Wachezaji wa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager wamefikia katika hoteli ya Pestana Rovuma mjini hapa baada ya kambi siku mbili Johannesburg, Afrika Kusini na wameonyesha hali ya kujiamini kuelekea mchezo huo.
Mbwana Samatta ataongoza safu ya ushambuliaji leo

Washambuliaji tegemeo wa Stars, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaochezea TP Mazembe ya DRC wamesema kwamba watajitolea kila kitu katika mchezo huo ili kuipa matokeo mazuri timu.
“Tunapita katika mtihani mgumu, si jambo zuri kuishia hapa katika mbio za AFCON, ambazo kwa miaka sasa tangu kizazi kilichopita tumekuwa tukisotea fainali zake. Tutapambana, tunaomba duwa za Watanzania tu,”alisema Samatta. 
Balozi wa Tanzania nchini hapa, Shamim Nyanduga amekuwa bega kwa bega na timu tangu imefika hapa akisaidia maandalizi ili kuiepusha na mitego ya hujuma za wenyeji, kuanzia chakula, usafiri hadi malazi.
Mechi hiyo itakayochezeshwa na waamuzi kutoka Uganda wakiongozwa na Dennis Batte itaanza saa 9:00 Alasiri kwa saa za hapa, saa moja zaidi kwa saa za nyumbani Tanzania.
Kikosi cha Stars kinatarajiwa kuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Said Mourad, Shomary Kapombe, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Erasto Nyoni, Thomas Ulimwengu, Mwinyi Kazimoto, John Bocco, Mbwana Samatta na Khamis Mcha ‘Vialli’.
Katika benchi wanatarajiwa kuwapo Aishi Manula, Aggrey Morris, Oscar Joshua, Haroun Chanongo, Mrisho Ngassa, Simon Msuva na Amri Kiemba. 
Wachezaji wengine waliopo hapa na timu ni Himid Mao, Shaaban Nditi na Ramadhani Singano ‘Messi’.
Katika mechi saba zilizopita baina ya timu hizo tangu mwaka 2006, Tanzania imeshinda moja tu, tena ya kirafiki Dar es Salaam 1-0 Novemba 19, mwaka 2008 wakati Msumbiji imeshinda mbili, moja ya kirafiki 2-0 Maputo Novemba 19, mwaka 2008 na nyingine ya kufuzu AFCON Septemba 8, mwaka 2007 Dar es Salaam wakati mechi nne zimetoka sare.
Mholanzi Nooij leo atakuwa anaiongoza Stars katika mechi ya saba tangu arithi mikoba ya Mdenmark, Kim Poulsen, akiwa amepoteza mechi moja tu, tena ya kirafiki 4-2 dhidi ya Botswana mjini Gaborone.
Khamis Mcha 'Viallia' ataaza leo badala ya Mrisho Ngassa 

Ametoa sare tatu dhidi ya Malawi 0-0 mchezo wa kirafiki mjini Mbeya, Zimbabwe 2-2 mjini Harare kufuzu AFCON na 2-2 tena dhidi ya Msumbiji kufuzu AFCON pia mchezo wa kwanza Dar es Salaam.
Ameshinda 1-0 mara mbili, dhidi ya Zimbabwe mjini Dar es Salaam kufuzu AFCON na Malawi mchezo wa kirafiki Dar es Salaam. 
Kihistoria, Tanzania imefuzu AFCON mara moja tu mwaka 1980 mjini Lagos, Nigeria, wakati Msumbiji imecheza Fainali nne za michuano hiyo katika miaka ya 1986, 1996, 1998 na 2010, zote wakitolewa hatua ya makundi kama Taifa Stars. Kila heri la Taifa Stars. Mungu ibariki Tanzania. Amin.

0 comments: