Na James Magai, Mwananchi
Dar es Salaam. Katibu wa Jumuiya na
Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda leo anatarajiwa kuwa na
kibarua kingine kigumu katika kupangua kigingi cha kufutiwa shtaka la
kukaidi amri ya mahakama, alichowekewa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Sheikh Ponda kwa sasa anasota mahabusu
kutokana na kesi ya jinai inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Morogoro, akidaiwa kufanya makosa ya uchochezi katika maeneo mbalimbali
mjini Morogoro na kukiuka amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
.
Hata hivyo Ponda kupitia kwa Wakili
wake Juma Nassoro, amewasilisha maombi ya marejeo, akiiomba Mahakama Kuu
ifanye marejeo ya uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro kukataa
maombi yake ya kumfutia shtaka hilo.
Maombi hayo yalitarajiwa kusikilizwa
na Jaji Agustine Mwarija juma lililopita lakini yaligonga mwamba baada
ya DPP kuwasilisha pingamizi mahakamani hapo akiiomba mahakama
iyatupilie mbali maombi hayo, pamoja na mambo mengine akidai kuwa,
yamewasilishwa kinyume cha sheria.
Kutokana na pingamizi hilo, Jaji
Mwarija aliahirisha usikilizwaji wa maombi hayo ya msingi hadi leo kwa
ajili ya kusikiliza pingamizi hilo la DPP.
Katika pingamizi hilo, DPP kupitia kwa
Wakili wa Serikali, Bernard Kongola alidai kuwa maombi hayo
yamewasilishwa kinyume na kifungu cha 372 (2) Sheria ya Mwenendo wa
Makosa ya Jinai (CPA).
Alidai kwa mujibu wa kifungu hicho mtu
haruhusiwi kuwasilisha ombi la marejeo ambayo yanatokana na uamuzi au
amri ya mahakama ya chini ambayo haimalizi kesi.
Hii ni mara ya pili kwa Sheikh Ponda
kuwasilisha mahakamani hapo maombi hayo baada ya Mahakama Kuu
kuyatupilia mbali kutokana na pingamizi lililowekwa na DPP.
Maombi hayo ya kwanza yalitupiliwa
mbali na Jaji Rose Teemba,Desemba 11, 2013, baada ya DPP kumwekea
pingamizi kuwa hati ya kiapo iliyokuwa ikiunga mkono maombi yake ilikuwa
na kasoro za kisheria
0 comments:
Post a Comment