Viongozi nchini Ukraine
Balozi wa Ukraine katika Umoja wa Mataifa ameomba kikao cha dharura cha Baraza la Usalama ili kufanya kila linalowezekana kuzuwia uvamizi wa Urusi, wakati vikosi vya jeshi la nchi hiyo vikidhibiti jimbo la Crimea.
Lakini hatua hazionekani kuwa zinaweza kuchukuliwa na chombo hicho chenye nguvu cha Umoja wa Mataifa. Kama mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama, Urusi ina nguvu za karata ya turufu na inaweza kuzuwia baraza hilo kuidhinisha azimio lolote litakalokosoa ama kuiadhibu nchi hiyo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amemtaka Rais Vladimir Putin katika mazungumzo kwa njia ya simu "kuanza mazungumzo ya ana kwa ana na maafisa wa serikali mjini Kiev."
Hali ni ya hatari Ukraine
Akiita hali nchini Ukraine kuwa "ya
hatari na inayodhoofisha amani", balozi wa Marekani katika Umoja wa
Mataifa, Samantha Power, ameliambia Baraza hilo kuwa "umefika wakati kwa
uvamizi wa jeshi la Urusi nchini Ukraine kusitishwa."
Power na wajumbe wengine wa Baraza
hilo wametoa wito wa kutumwa kwa wakaguzi wa kimataifa nchini Ukraine
haraka iwezekanavyo kuangalia hali nchini humo, na Power ameonya kuwa
"hatua za uchokozi za Urusi zinaweza kirahisi kuipeleka hali hiyo
kupindukia hali ya kuporomoka kabisa." Pia ametaja kuhusu kazi za ujumbe
wa upatanishi wa kimataifa kutumwa nchini Ukraine.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
limeitishwa kwa kikao cha dharura kwa mara ya pili mfululizo kuhusiana
na hali ya matukio inayokwenda kasi nchini Ukraine.
Baraza hilo pia lilikutana kwa muda
mfupi katika kikao cha wazi, kikao kilichoonyeshwa katika televisheni,
licha ya upinzani kutoka Urusi, na baadaye kilifanya tena mkutano wake
kwa faragha.
Obama aionya Urusi
Wakati huo huo, Rais Barack Obama
alimweleza Rais Vladimir Putin wa Urusi jana Jumamosi (01.03.2014) kuwa
hatua ya nchi hiyo kutuma wanajeshi nchini Ukraine ni kitendo cha
ukiukaji wa sheria za kimataifa na ameonya kuwa anatafakari kuitenga
nchi hiyo kisiasa iwapo hatua hiyo ya Urusi itaendelea.
Obama pia ameelezea kuhusu haki ya
watu wa Ukraine kuamua hatima yao na kuanza kimsingi kuwaweka pamoja
washirika wake wa mataifa ya magharibi dhidi ya Urusi, na kuwapigia simu
viongozi wa Ufaransa na Canada.
John Kerry, pia alifanya mazungumzo na
mawaziri wengine sita kutoka mataifa ya Ulaya na Canada pamoja na Mkuu
wa Sera za Mambo ya Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, pamoja
na balozi wa Japan nchini Marekani, kuratibu hatua itakayochukuliwa
baadaye.
Rais Obama alimpigia simu Rais
FrancoisHollande wa Ufaransa na Waziri Mkuu wa Canada, Stephen Harper,
viongozi wa mataifa ya upande wa pili wa Bahari ya Atlantic ikiwa ni
pamoja na Uingereza ambazo ni uti wa mgongo wa upinzani wa baada ya Vita
Vikuu vya Pili vya Dunia dhidi ya Urusi.
Canada kwa upande wake imesema
inamuondoa balozi wake kutoka Urusi kuhusiana na mzozo huo wa Ukraine.
Taarifa ya Waziri Mkuu Stephen Harper baada ya kikao cha dharura cha
baraza la mawaziri imesema Canada pia itasusia mkutano wa mataifa manane
tajiri utakaofanyika mjini Sochi nchini Urusi mwezi Juni.
Harper anashutumu vikali uingiliaji kati kijeshi wa Urusi nchini Ukraine na amemtaka Rais Putin kuondoa majeshi hayo.
Chanzo,dw.de/swahili
0 comments:
Post a Comment