Thursday, 6 March 2014

MAFANIKIO YA CHAMA KIKUU CHA USHIRIKA KAGERA YASIPOTOSHWE

 
Jengo la kisasa la KCU 1990 LTD (Bahaya building)
Jengo la kisasa la KCU 1990 LTD (Bahaya building).
Na Deogratias Kishombo
Pamoja na juhudi zote zinazofanywa na uongozi wa juu wa chama cha msingi Mkoa wa Kagera  kwa kushirikiana na wanachama wa zao la kahwa mkoani humo zinapigwa vita na baadhi ya watu wachache ambao kwa namna moja ama nyingine hawawatakii mema wakulima na familia zao  ambao wanategemea zao la kahawa  kiuchumi.
Kumekuwepo na  upotishaji wa makusudi hasa katika kutaka kufitinisha wakulima ambao wana imani na viongozi wao kuanzia ngazi ya chama cha msingi hadi chama kikuu cha ushirika (KCU 1990 Ltd)
Aidha KCU inategemewa na si wakulima pekee yake bali pia watu wengine wakiwepo wataalam waajiliwa kuanzia madereva, wafanyakazi wa maofisini, wataalam washauri, n.k
Ukiwasikiliza wakulima wenyewe ambao wanatoka katika mtandao wa vyama vya msingi zaidi ya 100 na pia viongozi hasa wa kiserikali mkoani Kagera watakuambia ni kuendelea kuchelewesha maendeleo katika Mkoa huo uliyoko kaskazini mwa Tanzania.
Wakulima wanaenda mbali zaidi kwa kusema, fitina hizo si tu zitaathiri wakulima pekee bali zitawagusa hata watu wengine na kwenye sekta ya kahawa mkoani humo . Wanasema kilimo cha kahawa kina changamoto nyingi hivyo si busara kuwashambulia viongozi wa ushirika bila kangalia masuala ya msingi kuanzia kwa mkulima mwenyewe.
Hoja hiyo inangwa mkono na Mbunge wa Muleba Kaskazini Charles Mwijage ambaye anasema kinachotokea sasa ndani ya ushirika wa Kagera ni changamoto ambazo zimejikita katika katika masuala mbalimbali kuanzia kwa mkulima mwenyewe.
“Suala lililopo katika ushirika wa Kagera ni changamoto ambazo zinahitaji kutatuliwa kuanzia kwa mkulima mwenyewe siyo viongozi waliopo madaraka” anasema na kuongeza.
“Lazima tuangalie mifumo yetu. Tuangalie tunapataje wawakilishi,  tunazalisha kiasi gani na kwa kiwango gani. Pia tuangalie mifumo yetu ya uwakilishi kama inakidhi matakwa na mambo kadha wa kadha, kuendelea kusema viongozi wetu hawatufai siyo suluisho la matatizo ya ushirika” anasema.
Naye Meneja Mkuu wa kiwanda cha kutengeneza kahawa cha Tanganyika Instant Coffee Company (Tanica) Bwana  Leonidas Ishansha anasema anawashukuru KCU kwa ubia wao na kwa kutoa mchango mkubwa kwa kiwanda hicho lakini anasema uzalishaji usioridhisha wa kahawa unaathiri mapato na uzalisha ji wa kiwanda hicho.  KCU inamiliki zaidi ya asilimia 50 ya kiwanda cha TANICA
“Uwezo wetu nikuzalisha tani 500 kwa mwaka lakini kutokana na uzalishaji mdogo tunazalisha chini ya kiwango karibu tani 300 kwa mwaka” anasema.
Bwana Ishansha amesema hayo baada ya Kampuni yake ya TANICA kupata tuzo   katika orodha ya makampuni bora ya kati (Mid-sized companies) mwaka 2013 mashindano ambayo yanaratibiwa na Kampuni ya kimataifa ya KPMG. TANICA imeibuka kampuni bora pekee kutoka katika mkoa wa Kagera.
“Mafanikio yetu yanatokana na juhudi za chama cha msingi cha mkoa wa Kagera yaani KCU 1990 ltd ambacho kimekuwa chanzo chetu kikuu cha fedha na pia wanatupatia kahawa kwa ajili ya uzalishaji” anaongeza.
KCU imekuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo ya mkoa ukianzia ngazi ya mkulima wa kawaida wa kahawa  hadi kwa pato la mkoa pamoja na kupitia katika changamoto mbalimbali.    
KCU 1990 Ltd imebuni miradi mingi katika mtandao wake wa vyama vya msingi kutoka katika wilaya za Misenyi, Muleba na Bukoba. Mtandao huu una vyama vya msingi 125 na wanachama zaidi ya 60,000.
 Katika juhudi hizo, kimebuni kuwasaidia wakulima wanaozalisha kahwa ya “organic” kwa kuwapatia mashine za kukoboa kahawa na kimewapatia wasimamizi wataalamu wa kuwasidia wakulima  katika maeneo yao ya kilimo.
Aidha, katika juhudi hizo KCU pia imebuni vyanzo mbalimbali vya mapato  ili chama kikuu hicho  kiweze kujiendesha na kuwasaidia wakulima. Kwa sasa KCU inamiliki mahoteli, viwanda, majengo na vyanzo vingine mbalimbali vya mapato ambavyo vinatoa ajira na kupunguza umasikini katika mkoa wa Kagera.
Baadhi ya wakulima wamenufaika na mikopo inayotolewa na vyama vya ushirika vya kuweka na kukopa (SACCOS) vilivyo chini ya KCU.
Kama anavyosema Meneja mkuu wa chama kikuuu cha ushirika mkoani humo  Vedastus Ngaiza, ushirika wa Kagera ndiyo ushirika pekee wa mfano ukilinganisha na mikoa mingine.
Ngaiza anamshukuru Rais Kikwete kwa juhudi zake za kuunga mkono ushirika wa Kagera. Rais Kikwete aliusifia ushirika wa Kagera wakati akizindua jengo la kitega uchumi cha KCU katikati ya mji wa Bukoba mtaa wa One way.
Bwana Ngaiza anasema “Tunashukuru kuona kwamba  viongozi wetu wa serikali na wakulima  wanatuunga mkono pamoja na kuwepo ghiriba za watu wachache. Hatutakata tamaa” anasema.
Anatoa ushauri kwa wakulima kwamba waendelee kuzalisha kwa kiwango kikubwa lakini wajitahidi sana kuzalisha kahawa bora.
“Ninawashauri wakulima wazalishe kahawa bora ili wajiongezee kipato kwa ajili ya familia zao na kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi” anaongeza.
Naye Mkuu wa mkoa wa Kagera Kanali mstaafu Fabian Masawe  chini ya kauli mbiu yake ya kuleta maendeleo “Kagera Amani na Maendeleo” anawashauri wanakagera kujikita katika masuala ya maendeleo  na kuacha masuala ya malumbano yasiyo kuwa na tija katika mkoa wa Kagera.
Akiongea na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake mjini Bukoba mwishoni mwa mwaka jana mkuu huyo wa Mkoa anasema, “Kagera ni mkoa uliobarikiwa kuwa na rasilimali nyingi  hivyo masuala yasiyokuwa na tija yanarudisha nyuma maendeleo” alisema.
Katika kipindi cha utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2012/2013, Mkoa wa Kagera ulikabiliwa na changamoto mbalimbali kubwa ikiwa Mwamko mdogo wa wananchi wa Kagera kuchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani humo.

0 comments: