Saturday, 1 March 2014

BUNGE LA KATIBA LAPINGWA

bungepic_85c1a.jpg
Dodoma. Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Mwalimu Nyerere Idealogy Conservation Society ya jijini Tanga, imefungua Kesi Mahakama Kuu ikitaka kuzuia mchakato wa Mabadiliko ya Katiba.
Taasisi hiyo inapinga mchakato huo wa Katiba kwa kile inachodai kuwa ni kasoro zilizojitokeza, ikiwamo wananchi kukosa uwakilishi uliotokana na ridhaa yao, posho kubwa wanayolipwa wajumbe na gharama kubwa zilizotumika katika maandalizi ya Bunge hilo.
Kesi hiyo ya madai namba 02/2014, ilifunguliwa Februari 17, mwaka huu katika Mahakama Kuu Kanda ya Tanga na mwenyekiti wa taasisi hiyo, Dk. Muzzammil Mussa Kalokola.
Washtakiwa katika kesi hiyo iliyofunguliwa kwa stakabadhi ya malipo ya Serikali namba 49803745, ni Waziri wa Sheria na Katiba, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), (kwa sasa ni Frederick Werema) na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo Mwenyekiti wake ni Jaji Mstaafu, Joseph Warioba.
Hata hivyo Jaji Werema na Jaji Warioba wamesema hawana taarifa za kesi hiyo.
Dk. Kalokola alisema katika hati yake ya madai kuwa anataka mchakato huo wa Katiba usitishwe kwa kuwa umevunja Katiba iliyopo.
Amesema Katiba ya sasa imekiukwa katika Muundo wa Bunge la Katiba na Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika utekelezaji wa majukumu na wajibu wake wa kukusanya maoni na kutengeneza Rasimu ya Madadiliko ya Katiba ibara ya 98.
"Vilevile imeshindwa kuzingatia hadidu za rejea kama zilivyoainishwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83," alisema Dk Kalokola.
Dk. Kalokola alifafanua kuwa Katiba ya sasa imeweka masharti kadhaa, ikiwamo utaratibu wa namna ya kuibadilisha na sheria nyingine ambazo zimeanishwa katika ibara ya 98 na Sheria ya mwaka 1984 Na.15 ib.14.
"Ibara ya 98 (1) Bunge laweza kutunga sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii kwa kufuata kanuni zifuatazo," alisema huku akiinukuu ibara hiyo na kuendelea:
"Muswada wa Sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii (isipokuwa yale yanayohusika na aya ya (b) ya ibara hii ndogo) au masharti yoyote ya sheria yoyote iliyotajwa katika orodha ya Kwanza kwenye Nyongeza ya Pili utaungwa mkono kwa kura za wabunge ambao idadi yao haipungui theluthi mbili ya wabunge wote.
"Muswada wa sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii au masharti yoyote ya sheria yoyote yanayohusika na jambo lolote kati ya mambo yaliyotajwa katika Orodha ya Pili kwenye Nyongeza ya Pili iliyoko mwishoni mwa Katiba hii, utapitishwa tu iwapo utaungwa mkono kwa kura za wabunge ambao idadi yao haipungui theluthi mbili ya wabunge wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wabunge wote kutoka Tanzania Zanzibar."
Alisema kwa madhumuni ya ufafanuzi wa masharti ya ibara ndogo ya (1) "kubadilisha masharti ya Katiba hii au masharti ya sheria maana yake ni pamoja na kurekebisha au kusahihisha masharti haya au kufuta na kuweka masharti mengine badala yake au kusisitiza au kubadilisha matumizi ya masharti hayo".
"Pingamizi limepelekwa mahakamani kutokana na tume kushindwa kuzingatia masharti ya Katiba yaliyowekwa na ibara hii, ibara ya 98. Vilevile tume imeshindwa kuzingatia masharti ya hadidu za rejea yaliyowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba sura 83," alisema.
Kwa mujibu wa Dk Kalokola, katika kutunga sheria ya kuunda Bunge la Katiba Serikali imelipotosha Bunge kwa kuunda sheria ambayo haikuzingatia masharti ya uhalali wa uwakilishi kama yalivyowekwa na Katiba hususan ibara ya 21.
"Kwa mujibu wa uhalali wa uwakilishi, Katiba inaweka masharti kuwa wawakilishi halali watakuwa ni wale waliochaguliwa na wananchi kwa hiari yao, kwa haki na uhuru kabisa kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria," ameeleza katika hati hiyo na kuendelea;
"Baya zaidi Mheshimiwa Rais aliahidi kuwa kwa mujibu wa sheria uteuzi utalenga kutengeneza Bunge la Katiba lenye sura ya utaifa kwa kuzingatia mahali wanapoishi wajumbe walioteuliwa. Kwa uhalisia wajumbe kutoka Tanzania Bara, zaidi ya asilimia 75 wanaishi Dar es Salaam."
Dk. Kalokola ameeleza pia kuwa Serikali iliwapotosha wabunge kutokana na shinikizo la wanaharakati kutunga sheria ambayo inawapa nafasi wanaharakati kushiriki katika uamuzi wa Katiba ambayo wananchi wangeipenda.
"Ifahamike kuwa asasi zote za wanaharakati zimeundwa kwa malengo ya kushinikiza Serikali kukubali matakwa ya masilahi yao. Baya zaidi wanaharakati wengine ni mawakala wa wakoloni mamboleo kutoka nchi za nje," alisema.
Dk. Kalokola alieleza kuwa kesi hiyo imefunguliwa kupinga posho zilizoahidiwa kwa wajumbe wa Bunge la Katiba, kwa kuwa ni kubwa mno ikilinganishwa kipato cha taifa.
"Tukumbuke kuwa Serikali imepuuza kuwa ina dhima kubwa kwa ustawi wa jamii, na wafanyakazi wengine kama walimu hawajalipwa stahiki zao. Serikali imefanya makosa kutumia fedha kuwa silaha yetu ya kupata Katiba Mpya. Ifahamike kuwa Baba wa Taifa alisema kuwa ni fikra potofu kuchagua fedha kuwa silaha yetu, silaha ambayo hatuna. Mnyonge hawezi kuchagua fedha kuwa silaha yake," alisema.
Ombi mahakamani
"Tumeiomba Mahakama itoe tamko la kuwalazimisha wahusika kuzingatia masharti yaliyowekwa na Katiba katika utekelezaji wa majukumu na wajibu wao na kusimamisha Bunge la Katiba hadi hapo litakapopatikana Bunge la Katiba lenye uhalali wa uwakilishi litakolokuwa limechaguliwa na wananachi wenyewe kwa hiari yao kwa haki na uhuru kabisa," alisema.
Dk. Kalokola alieleza kuwa uongozi siyo kazi na Serikali imekosea kupuuza uzalendo na kutanguliza fedha.
Chanzo: Mwananchi

0 comments: