Monday 30 June 2014

YANGA YASHANGAA NGASSA KWENDA BONDENI! SOUTH AFRIKA

 
KATIBU MKUU wa Yanga, Beno Njovu, ameripotiwa kushangazwa na taarifa kuwa Straika wao Mrisho Ngassa alikwenda Afrika Kusini kwa Majaribio na Klabu ya Free State Stars FC.
Njovu alisema kuwa walichokuwa wanajua wao ni kuwa Free State Stars FC walionyesha nia ya kumtaka Straika huyo mahiri na wakapewa masharti ya kumnunua.
Miongoni mwa hayo ni kutaka Klabu hiyo ya Afrika Kusini isubiri hadi Ngassa atakaporudi Nchini, akitokea Botswana alikotakiwa kuwepo kwenye Kambi ya Taifa Stars kama wao Yanga walivyofikiria ndiko yuko, ili wazungumze nae kuona kama ataikubali Klabu hiyo ili waendelee na majadiliano ya Uhamisho.
Njovu alitoboa kuwa hapo Juni 20 waliwaambia Free State Stars FC kuwa thamani ya Ngassa ni Dola 150,000.
Njovu alieleleza: “Tulichokuwa tunajua ni kuwa Ngassa yuko na Timu ya Taifa huko Botswana na hatujui lolote kwenda huko Afrika Kusini kufanya Majaribio na kufuzu upimwaji afya!”
‘WAPINZANI’ YANGA WAINGIA MITINI KUJIANDIKISHA!
MSEMAJI wa Klabu ya Yanga, Baraka Kizuguto, amesema Zoezi la Kuandikisha Wanachama wao wanaopinga Mwenyekiti Yusuf Manji kuongezewa Mwaka mmoja kwenye uongozi na ndipo ufanyike Uchaguzi Mkuu limefungwa.
Kizuguto alisema Zoezi hizo limefungwa baada ya Siku 5 zilizotolewa kufanywa Uandikishwaji kumalizika bila ya ‘Wapinzani’ hao kujitokeza.
Mwenyekiti Manji alipitishwa na Wanachama 1522 kwenye Mkutano Mkuu wa Yanga uliofanyika hivi karibuni kuendelea kukaa madarakani kwa Mwaka mmoja zaidi na kisha ufanyike Uchaguzi Mkuu lakini baadae kukaibuka Kikundi kilichopinga hilo.
Ndipo Manji akaamua ‘Wapinzani’ hao wajiandikishe na ikiwa watafika idadi ya 1522 basi yeye ataitisha Mkutano Mkuu wa Uchaguzi.
Kizuguto amesema suala hilo sasa limefungwa na wao wanaelekeza nguvu zao kwenye Usajili wa Wachezaji pamoja na maandalizi ya Msimu mpya wa Ligi unaoanza Agosti 24.

0 comments: