Thursday 26 June 2014

MCHANGO WA VIONGOZI WA DINI KATIKA MASUALA YA KIJAMII


1 
Meza Kuu wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki. 7 
Makamu wa Rais Dk. Mohamed Bilal akiagana na mwenyeji wake Askofu  Mkuu wa KKKT Dk. Alex Malasusa.
………………………………………………………………..
Hussein Makame-MAELEZO
MCHANGO wa viongozi wa dini katika jamii yoyote ile umekuwa ukipewa nafasi kubwa hasa katika muktadha wa ujenzi wa jamii bora yenye amani, maelewano usawa na maendeleo.
Katka miaka ya hivi karibuni baadhi ya nchi za Ukanda wa Jangwa la Sahara kama si za Afrika kwa ujumla zimekuwa zikikabiliwa na changamoto ya migogoro inayochangiwa na ama siasa za nchi husika na tofauti za kidini.
Baadhi ya migogoro hiyo ni ile inayotokea katika nchi kama za Nigeria, Sudan Kusini, Somalia ambapo baadhi ya makundi mbalimbali yamekuwa yakipigana ama kutokana na sababu za kisiasa au kidini.
Kutokana na hali hiyo viongozi wa dini kutoka nchi za Afrika ikiwemo ukanda wa Jangwa la Sahara walikutana hivi karibuni kwenye Mkutano wa Kimataifa la Viongozi wa Kidini kuhamasisha Amani, Demokrasia na Maendeleo.
Katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam, mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal huku wadau mbalimbali wa masuala ya Amani, Demokrasia na Maendeleo walialikwa na kuwasilisha mada mbalimbali.
Baadhi ya wadau hao ni viongozi kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tanzania Labour Party (TLP), Chama cha Wananchi (CUF) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Wakati akifungua mkutano huo Makamu wa Rais Dk. Bilal anawataka viongozi wa dini kuacha woga na kuwakemea viongozi wa kisiasa wanapokosea kwa kufanya hivyo wataendeleza amani iliyopo nchini na katika baraza zima la Afrika.
Dk. Bilali alisema Serikali ipo tayari kupokea mapendekezo watakayoyatoa kwa lengo la kudumisha amani na demokrasia kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla na kubainisha kuwa amani inajengwa kwa ushirikiano wa viongozi wa dini, wanasiasa na wadau wengine katika jamii.
Makamu wa Rais anasema kutokana na utayari huo ni vyema viongozi wa dini wakawakumbusha wanasiasa pale wanapokesea ili wajirekebisha na hivyo kuiepusha jamii kuingia katika uvunjifu wa amani.
Akizungumzia kongamano hilo Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dkt. Alex Malasusa anasema lengo la mkutano huo ni kuwakumbusha viongozi wa dini na wa siasa kuhusu suala la kudumisha amani kwani bila ya amani hakuna maendeleo.
“Nia ya mkutano huu ni kuwakumbusha viongozi wa dini kuhusu suala la kudumisha amani na nafasi ya viongozi wa dini kuombea amani na kuwakumbusha viongozi wa siasa wajibu wao katika kudumisha amani kwa sababu bila ya amani hatuwezi kupata maendeleo” anasema Dkt. Malasusa.
Katibu Mkuu wa CHADEMA Dkt. Wilborad Slaa alikuwa miongoni mwa washiriki waalikwa wa mkutano huo, anasema katika dhana ya maendeleo na amani anakubaliana na hoja kwamba iwapo amani haitakuwepo maendeleo hayawezi kupatikan
“Ni kweli kwamba iwapo amani haitakuwepo maendeleo pia hayatakuwepo, mimi nashukuru tumeunganisha amani, demokrasia na maendeleo kwa sababu kila kimoja kati ya mambo hayo kinategemea kuwepo kwa kingine” anasema Dkt. Slaa.
Kwa kutambua umuhimu wa mkutano huo, washiriki kutoka mataifa ya Ethiopia, Kenya, Nigeria, Afrika Kusini na mweneyji Tanzania hatimaye walitoka na tamko juu ya mambo yanayoweza kuchangia kuwepo kwa Amani, Demokrasia na Maendeleo
Mambo hayo ni katiba za nchi na uhuru wa dini katika ukanda wa Jangwa la Sahara, Hali tete ya sasa ya uhusiano kati ya wakristo na waislamu,mchango wa viongozi wa dini katika demokrasia na utawala bora na tamko la kuangalia fursa za kupunguza umasikini kama njia ya kupata amani na maendeleo.
“Tunakiri kwamba tofauti za kidini zimekuwa zikitumiwa vibaya na kwamba matumizi haya mabaya yamechangia kuvunja amani na hata kupoteza maisha ya watu na hivyo kuongeza umasikini” inafafanua sehemu ya tamko hilo.
Washiriki wa mkutano huo pia wamekubaliana kwamba wametambua na kukubali ukweli kwamba wao kama viongozi wa dini na siasa, ni jukumu lao kujenga na kuhamasisha thamani ya demokrasia.
Kama ishara ya matokeo yenye matumaini mema ya mkutano huo na “Tunakiri umoja kati yetu katika kudumisha amani, kuhamasisha demokrasia na kuhakikisha tunakuwa na uhakika wa maendeleo endelevu ambayo ni rafiki wa mazingira katika nchi za Ukanda wa Jangwa la Sahara na Afrika kwa ujumla.
“Tumejitolea kuhamasisha watu kuwa mstari wa mbele kujenga amani, demokrasia na maendeleo na kuhamasisha usawa wa kijinsia katika jamii.Kuwahamasisha wanajamii kujenga daraja katika kufahamiana miongoni mwa watu wa dini na kujihusisha katika mahusiano ya kidini.
“Kushirikiana na viongozi wa kisiasa kufanya kazi kwa ajili ya haki ya kijamii na kiuchumi kama mahitaji ya kujenga amani na kukabiliana na hali tete ya kidini kabla ya kugeuka vurugu na kupinga majaribio yote yanayofanywa na mtu au kikundi chochote kutumia vibaya dini na au siasa kwa manufaa binafsi au ya kisiasa” inasema sehemu ya tamko ambalo lilisainiwa na washiriki 31.
Washiriki wa mkutano huo pia wamekubaliana kutambua na au kulaani vurugu zote dhidi ya jamii yoyote na wameahidi kutumia jukwa lao kama viongozi wa dini katika kuhamasisha utawala bora.
Mambo mengine waliyokubaliana ni kuboresha na kuendeleza majukwaa ya mahusiano au maingiliano ya kidini kwa ngazi zote kwa kuhamasisha ujenzi wa amani, demokrasia na maendeleo ili kuchangia kupunguza umasikini.
Tamko hilo limetaka kuhamasisha uelewa wa mahusiano ya kidini katika mfumo rasmi wa mafunzo kwa viongozi wa dini na kuhamasisha mahusiano endelevu ya kidini na kukuz dhana ya ukarimu.
Kwa mujibu wa tamko hilo, washiriki wametaka itambulike ukweli ni kwamba ujenzi wa amani ni suala mtambuka na ili kuhamasisha uwepo wa amani, tunatoa wito kwa wadau wote ikiwemo Serikali, taasisi binafsi, wanasiasa, wasomi na jamii kwa ujumla kuheshimiana na kujenga dhamira ya kujiletea maendeleo endelevu.
“Kuheshimu kuwepo kwa tofauti za kidini kama zawadi na isiwe kikwazo cha kupata amani na kudumisha na kuheshimu kanuni za demokrasia kama mchakato wa kudumisha haki ya kila mtu” inafafanua sehemu ya tamko hilo.
Kwa pamoja viongozi hao wamekubaliana kwamba viongozi wa dini wana wajibu wa kuepuka kuendeleza uungaji mkono katika agenda za kisiasa na  kufanyia kazi mifarakano na machafuko ya kidini.
Mkutano huo ulidhaminiwa na Shirikisho la Kilutheri Duniani (LWF), Mfuko wa Konrad Adenauer (KAS), Kanisa la Evangelical Lutheran la Tanzania na Mission EineWelt, kwa ushirikiano na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).
Taasisi nyingine katika mkutano huo uliokuwa na kaulimbiu isemayo “Ujenzi wa Amani, Demokrasia na Maendeleo:Ni Wito  kwa Wananchi wa Ukanda wa Jangwa la Sahara”. Ulihudhuriwa pia na Ofisi ya Mufti ya Zanzibar na Chama cha Maendeleo ya Asia Tanzania (TADA)

 Picha zote na Hussein Makame-MAELEZO

0 comments: