Saturday 28 June 2014

SUAREZ: URUGUAY YAKATA RUFAA, SUAREZ ADAI HAKUUMA, ALIANGUKA!


FIFA imethibitisha kuwa Uruguay imekata Rufaa kwao kupinga kufungiwa kwa Straika wao Luis Suarez kwa kosa la kumuuma Meno Mchezaji wa Italy Giorgio Chiellini wakati wa Mechi ya Kombe la Dunia huko Brazil.
Uamuzi wa kukata Rufaa ulipelekwa FIFA Jana na Chama cha Soka cha Urguay.
Mkuu wa Habari wa FIFA, Delia Fischer, amesema: “Tumepokea azimio toka Uruguay kwamba watakata Rufaa. Walituambia Jana jioni. Sababu za kukata Rufaa zinatakiwa ziwasilishwe kwa maandishi ndani ya Siku 7.”
Suarez amefungiwa na FIFA Miezi minne kutojihusisha na chochote kuhusu Soka ikiwemo kutokanyaga Mazoezi na kutoingia Uwanja wowote wa Mpira na pia kutocheza Mechi 9 za Kimataifa za Uruguay pamoja na kupigwa Faini ya Dola 111,000.SUAREZ-URUGUAY28JUN
Wakati huo huo, Barua ya Suarez iliyowasilishwa kwa Kamati ya Nidhamu ya FIFA kama utetezi wake kwa kosa hilo la kumuuma Meno Chiellini imedai hakumuuma Meno ila aliteleza na kumwangukia Mpinzani wake.
Barua hiyo imesema: “Haikutokea kama mlivyoeleza kwamba nilimuuma au nilikusudia kumuuma…..Niliteleza na kumwangukia Mpinzani wangu. Uso wangu ukamgonga na kuaacha mchubuko shavuni kwangu na maumivu makali kwenye Jino langu.”
Hata hivyo, Jopo la Watu 7 la Kamati ya Nidhamu ya FIFA liliukataa utetezi huo na kuamua kuwa aliuma ‘akiwa na nia, makusudi na bila kuchokozwa.’
Pia Jopo hilo lilithibitisha kuwa Refa wa Mechi hiyo, Marco Rodriguez wa Mexico na Wasaidizi wake wawili, hawakuliona tukio hilo kwa vile Mpira ulikuwa eneo jingine wakati huo.
Jopo hilo la Kamati ya Nidhamu ya FIFA lilikuwa chini ya Mwenyekiti, Claudio Sulser, Mchezaji wa zamani wa Kimataifa wa Switzerland, akisaidiwa na Wajumbe kutoka Cook Islands, Hong Kong, Pakistan, Panama, South Africa na Singapore.

0 comments: