Wednesday 21 May 2014

MRISHO KHALFAN NGASSA ALAMBA MAMILIONI


WAKATI wachezaji wengine wanavuna fedha za usajili katika kipindi cha kuelekea dirisha kuu la uhamisho, Mrisho Khalfan Ngassa ambaye yumo ndani mkataba na klabu yake, Yanga SC naye amevuna mamilioni kimtindo mwingine.
Kwa pamoja, Ngassa na mchezaji wa Yanga SC na timu ya taifa, Taifa Stars jana wamefanya tangazo la magodoro ya Comfy, ambayo yamewafanya wavune mamilioni.
Kiasi gani wamepata? Siri yao, lakini mbali na wao, mshambuliaji wa timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars, Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’ na winga wa Simba SC, Ramadhani Singano ‘Messi’ nao pia wameshiriki tangazo hilo kwa pamoja mwigizaji  Ahmed Ulotu ‘Mzee Chilo’.
Dili la mahela; Mrisho Ngassa kulia akiwa Deo Munishi 'Dida' katika na Mwanahamisi Omar 'Gaucho' na godoro la Comfy baada ya kumaliza kufanya tangazo la bidhaa hiyo
Watu pesa; Kulia kabisa Mzee Chilo ambaye naye ameshiriki tangazo hilo
Tangazo la Comfy ni mwendelezo wa Ngassa ‘kujipigia fedha’ katika sekta hiyo, baada ya awali kulamba bingo za matangazo ya Vodacom, Coca Cola, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na Wizara ya Maliasili na Utalii. Tangazo la Utalii alilokwenda kufanya Marekani akiingia uwanjani kuichezea Seattle Sounders kwa dakika saba ikicheza na Manchester United ya England mchezo wa kirafiki ndilo ambalo lilimuingizia fedha nyingi zaidi Ngassa.  Dida, Ngassa na Messi wote wapo katika kambi ya Taifa Stars ambayo leo inahamia Mbeya kwa maandalizi ya mchezo wa marudiano dhidi ya Zimbabwe wiki ijayo. Tanzania ilishinda 1-0 katika mchezo wa kwanza wa mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika 2015 nchini Morocco. Katika mchezo wa marudiano, Stars itahitaji kulazimisha sare ugenini mjini Harare Juni 1, ili kuingia hatua ya mwisho ya mchujo. 

Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam

0 comments: