Friday 23 May 2014

MAKAMU WA RAIS ZANZIBAR AWATAKA VIONGOZI KUACHA UCHOCHEZI WA MIGOGORO YA ARDHI

 
??????????????????????????????? 
Na Miza Kona – Maelezo Zanzibar 
MAKAMU wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd amewataka viongozI kuacha   uchochezi wa migogoro ya ardhi baina ya wananchi na wawekezaji kwa lengo la kujipatia manufaa yao .
Wito huo ameutoa huko Baraza la Wawakilishi Chukwani wakati alipokuwa akifanya majumuisho ya majadiliano ya bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa Fedha 2014/2015.
amesema kuna baadhi ya viongozi wanawachochea wananchi kufanya migogoro kwa sababu za kisiasa kitendo ambacho kinapelekea kukosa maendeleo ya nchi.
“Tuache kuchochea wananchi kufanya migogoro,pia tuache kuchochea wananchi na wawekezaji kwa lengo la kuleta maendeleo ya nchi ili serikali ipate pato na wananchi wapate ajira na kukuza uchumi”, alifahamisha Balozi Seif.
Balozi Seif amewasisitiza viongozi kuwashajihisha wananchi kuleta maendeleo na kuepuka Uchochezi wa kisiasa kwa lengo la kukuza uchumi ili jamii iweze kuhamasika na kudumisha amani.
Aidha Makamo wa Pili wa Rais amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wa siasa kutaja Majina ya viongozi wanapokuwa katika majukwaa ya kisiasa badala yake wanadi sera za vyama vyao.
Amesema viongozi wanapokuwa katika majukwaa ya siasa wanatakiwa kuwaelimisha wananchi mambo ya maendeleo ya nchi na sio kujadili kwa kuwataja majina watu kwani kufanya hivyo ni kuhatarisha amani na utulivu uliopo.
“Ili amani na utulivu iendelee nchini basi ni lazima wanasiasa kuachana na tabia ya kujadili na kutajana majina ya watu katika majukwaa ya siasa, mnatakiwa kukaa kwenye majukwaa kunadi sera za vyama na kuwaelimisha wananchi jinsi ya kuleta maendeleo ya nchi”, alisisitiza Balozi Seif.
Aidha Makamo huyo amefahamisha kuwa fedha za serikali zinatumika ipaswavyo kama zilivyopangwa kinyume na baadhi ya watu wanavyodai kuwa zinatumika kinyume na mahitaji yaliyopangwa.
Mapema akifanya majumuisho hayo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mohammed Aboud Mohammed amewataka wajumbe hao kushirikiana kwa pamoja na kuachana na malumbano ili kuweza kuimarisha uchumi wa nchi.
Aidha amefahamisha kuwa ni vyema kuimarisha Muungano na kujadili mambo ya msingi kwa  kuondoa kero zilizopo kwa kujenga hoja zitakazopelekea kupatikana Katiba bora.
Wajumbe hao wameipitisha vifungu vya bajeti ya Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais kwa mwaka fedha 2014/2015 kwa kuidhinisha jumla ya Shl. 19,988,300,000.

IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

0 comments: