Saturday 24 May 2014

KIONGOZI WA UKAWA ATIWA MBARONI

 
Wananchi wakifuatilia mkutano wa hadhara wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) uliofanyika juzi eneo la Polisi Nguruka, Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma. Picha na Ibrahim Yamola
Wakati Polisi mkoani Kigoma wakiwa wamemtia nguvuni Katibu Mkuu wa chama cha NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe kwa tuhuma ya kumdhalilisha Rais Jakaya Kikwete, Kiongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Profesa Ibrahimu Lipumba amesema hawatarudi bungeni mpaka kiongozi huyo wa nchi aombe radhi.
Nyambabe alikamatwa juzi saa 5 usiku katika Kijiji cha Nguruka Wilaya ya Uvinza mkoani humo saa kadhaa baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara wa UKAWA uliohutubiwa na Nyambabe na viongozi kutoka vyama vya Chadema na CUF.
Akiwahutubia mamia ya wakazi wa Nguruka katika mkutano wa Ukawa wenye lengo la kuwaelimisha wananchi kuhusu mchakato wa Katiba, Nyambabe alisema Rasimu ya Katiba ikipita kuwa Katiba, mamlaka ya uteuzi wa ovyo haitakuwapo tena.
"Jaji Warioba (aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba) ameweka mamlaka ya uteuzi kwenye Rasimu ya Katiba na Rais hataweza tena kuteua marafiki zake, shemeji zake, watu wake wa karibu kuwa viongozi mbalimbali hadi taratibu za ajira zifuatwe.
"Hivi sasa kuna mawaziri mizigo walioteuliwa na Rais (Kikwete) ambao wanalalamikiwa na chama chake (CCM) kushindwa kutekeleza majukumu yao na hii inatokana na kupeana madaraka kwa njia zisizo stahili," alisema Nyambabe.
Polisi wamdaka
Baada ya kumalizika mkutano huo, Nyambabe akiwa ameambatana na Mwenyekiti wa Vijana Taifa wa Chadema, John Heche na Mjumbe wa Baraza Kuu la CUF, Ashura Mustapha walikwenda hoteli waliyofikia ya New Gevena.
Ilipofika saa 5 usiku askari kanzu wanne walifika hotelini hapo wakiwataka viongozi hao kwenda Kituo cha Polisi Nguruka kwa madai ya kufanya uchochezi.
Walipofika walimwambia mhudumu wa hoteli hiyo kuwa wanawataka viongozi hao na aliwajibu hawapo jambo lililowafanya kumtaka kuwapa kitabu cha wageni wa siku hiyo.
Walipopewa kitabu walikuta jina la Nyambabe kuwapo hotelini hapo, Heche na Ashura wakiwa wameondoka kwenda Kigoma Mjini.
"Wakati askari hao wanne wapo ndani ya hoteli, nje kulikuwa na askari sita wenye silaha wakiwa wameizunguka hoteli hiyo na kumchukua kisha kwenda naye moja kwa moja Kituo cha Polisi Nguruka," alisema Mohamed Mtulya ambaye ni Ofisa Usalama wa NCCR-Mageuzi. 
 CHANZO:MWANANCHI

0 comments: