Wednesday 21 May 2014

MBEYA CITY WANACHEZA MECHI YA KWANZA KESHO SUDAN, LAKINI HADI SASA BADO WAPO DAR

HATA TIKETI HAWAJAPATA


HATMA ya safari ya timu ya Mbeya City kutoka jijini Mbeya kuelekea  Sudan kwa ajili ya kushiriki mashindano mapya ya Kombe la Nile Basin ambayo yanatarajiwa kuanza leo mjini Khartoum haijajulikana imeelezwa.
Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe, aliiambia BIN ZUBEIRY kuwa hadi leo mchana walikuwa hawajapokea tiketi hizo za kuelekea Sudan ili kupeperusha vyema bendera ya Tanzania Bara katika mashindano hayo.
Kimbe alisema kuwa timu yao inaendelea na mazoezi yake kwenye Uwanja wa Karume, Ilala jijini na mara safari hiyo itakapokamilika wataondoka kuelekea Sudan.
Wapo Dar; Mbeya City inatakiwa kucheza mechi ya kwanza kesho Sudan, lakini hadi sasa hawajapata hata tiketi na wapo Dar es Salaam

"Yaani hadi muda huu (jana mchana) bado hatujaambiwa chochote, timu inaendelea na mazoezi huku tukisubiri kupewa maelekezo na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambao ndiyo wanawasiliana na viongozi wa Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
BIN ZUBEIRY pia ilipomtafuta Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye, kutaka kufahamu hatma ya safari ya Mbeya City, kiongozi huyo ambaye ni Mkenya, hakupatikana katika simu yake ya mkononi.
Hata hivyo inaelezwa kuwa Chama cha Soka cha Sudan (SFA) ndiyo wanaotakiwa kushughulikia tiketi za timu na viongozi wanaoelekea nchini humo kwa kushirikiana na serikali yao iliyodhamini michuano hiyo.
Mechi za ufunguzi za mashindano hayo leo zitakuwa ni kati ya Victoria University dhidi ya Malakia na baadaye usiku wenyeji El Mereikh itawakaribisha Polisi kutoka Uganda timu hizo zote ziko kundi A.
Timu nyingine zinazoshiriki mashindano hayo zilizoko kundi C ni pamoja na Al Ahly Shandy, Al Masry ya Misri, Defence na Dhikil huku kundi D likiwa na Hey Al Arab, Arab Contractors, Flam beaude L'EsT ya Burundi na Etincelles ya jijini Kigali, Rwanda.
Mbeya City ambayo iko kundi B inatakiwa kuanza kampeni za kuwania ubingwa huo kesho Alhamisi kwa kuwavaa El Mereikh Al Fashery na baadaye kucheza na AFC Leopald ya Kenya Mei 25 na kumaliza mechi zake za hatua ya makundi kwa kukutana na Elman ya Somaliza Mei 27. 
 
Na Samira Said, Dar es Salaam
 

0 comments: