Friday 23 May 2014

ATCL YAREJEA KATIKA ANGA ZA ARUSHA,ZANZIBAR

 
ATCL 1 (1)  
Kaimu Mkurugenzi wa Biashara wa Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL) Bw. Juma Boma (kushoto) akiteta jambo na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Lazaro Nyalandu wakati wa uzinduzi wa safari ya ATCL ya Dar es Salaam -Arusha – Zanzibar, wakitumia ndege yao yenye uwezo wa kuwabeba abiria 50 aina ya Bombardier Dash-8. Uzinduri ulifanyika Jumatano jioni. (Picha na mpiga picha wetu) ATCL 2 
 Kaimu Mkurugenzi wa Biashara wa Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL) Bw. Juma Boma (wa kwanza kulia) akishuka kutoka katika ndege ya shirika hilo aina ya Bombardier Dash-8 akifuatwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Lazaro Nyalandu (wapili kulia) wakati wa uzinduzi wa safari za ndege hiyo kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar ikipitia Arusha. Hafla hiyo ilifanyika Jumatano jioni. (Picha na mpiga picha wetu) ATCL 3  
Kapteni Richard Shaidi (kulia) akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Lazaro Nyalandu (kushoto) mara tu baada ya ndege ya Air Tanzania (ATCL) kutua katiwakati uwanja wa ndege wa  Arusha ikiwa ni uzinduzi wa safari yake ya kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar ikipitia Arusha. Shirika hilo la ndege limepanga kusafiri mara sita kwa wiki ikitumia ndege yake ya aina ya Bombardier Dash-8. (Picha na mpiga picha wetu). ATCL 4  
Kaimu Mkurugenzi wa Biashara wa Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL) Bw. Juma Boma (kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa safari ya ATCL ya Dar es Salaam- Arusha – Zanzibar, wakisafiri mara sita kwa wiki kwa kutumia ndege yao ya aina ya Bombardier Dash-8. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini Bw. John Mongela. (Picha na mpiga picha wetu). ATCL 5 
 Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini Bw. John Mongela (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) maara baada ya kupokea wageni na abiria waliosafiri na ndege ya Air Tanzania, Jumatano jioni wakati wa uzinduzi wa safari ya ATCL ya Dar es Salaam -Arusha– Zanzibar, wakitumia ndege yao ya aina ya Bombardier Dash-8. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Biashara wa Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL) Bw. Juma Boma. (Picha na mpiga picha wetu). ATCL 6Kaimu Mkurugenzi wa Biashara wa Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL) Bw. Juma Boma (kulia) akibadilisha kadi ya mawasiliano na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora)-wa Zanzibar- Dk. Mwinyihaji Haji Makame (kushoto) aliyekuwa miongoni mwa abiria waliopanda ndege hiyo Jumatano jioni wakati wa uzinduzi wa safari ya ATCL ya Dar es Salaam- Arusha– Zanzibar ikitumia ndege yake ya aina ya Bombardier Dash-8. (Picha na mpiga picha wetu).
Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Ndege la Taifa, Air Tanzania (ATCL) limerejea katika anga za Arusha na Zanzibar na kuahidi kusafiri katika maeneo hayo yenye vivutio bora vya kiutalii mara sita kwa wiki.
Katika safari hiyo ya uzinduzi ya kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar kupitia Arusha, kulikuwa na mawaziri wawili wa pande zote za muungano ambao walionyesha kufurahishwa na safari hiyo, mbali na kutoa nasaha kwa shirika hilo.
Ikitokea Dar es Salaam kwenda Arusha, alikuwemo Waziri wa Maliasili na Utalii Bw. Lazaro Nyalandu na wakati wa kutoka Zanzibar kwenda Dar es Salaam, alipanda Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Zanzibar (Utawala Bora), Dkt. Mwinyihaji Haji Makame, wote wakiashiria kuwa safari hiyo imerejesha matumaini ya kuwaunganisha watalii kutoka Arusha kwenda Zanzibar na kurudi Dar es Salaam.  
Akizungumza mara baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa Arusha, Mh. Nyalandu, alisema kurejea kwa ndege ya shirika hilo la Taifa katika njia ya Arusha na Zanzibar kutakuza sekta ya utalii na kurahisisha uunganishwaji wa maeneo hayo muhimu yenye vivutio vikubwa vya utalii.
“Ninayofuraha ya kuwataarifu watalii, wageni wanaotembelea nchi yetu na watanzania wenzangu kuwa Air Tanzania sasa imerudi angani. Nimekuwa miongoni mwa abiria wa kwanza kusafiri na ndege hii kuja hapa Arusha, kwa hiyo nataka kuwahakikishia wote kuwa usafiri wa Air Tanzania ni tulivu, wanatoa huduma nzuri ndani ya ndege, ni salama na utafurahia safari yako.
“Uzinduri wa safari hii unadhihirisha kwamba sasa ushindani wa kweli katika sekta ya usafiri wa anga umeanza. Shirika la Air Tanzania linatakiwa kuhakikisha linaendeleza dhamira yake ya kutoa huduma bora ili liweze kurejesha imani lililokuwanayo kwa abiria wake walio wengi,” alisema Nyalandu.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Biashara wa ATCL Bw. Juma Boma alisema safari ya Dar es Salaam – Arusha – Zanzibar ni sehemu ya mkakati wa shirika lake wa kutanua huduma zake katika maeneo mengi iwezekanavyo.
“Tunajivunia kuendelea kutekeleza dhamira yetu ya kuimarisha huduma zetu tukiwa kama shirika la Ndege la Taifa. Tukilenga kuendelea kutanua wigo wa huduma zetu ndani ya nchi na kimataifa.
“Lengo letu kubwa kama Shirika la Ndege la Taifa ni kuendelea kutoa huduma zenye gharama nafuu, vile vile kuongeza uwezo wa abiria kusafiri kwa wakati wao”. Ndiyo sababu tumeondoa adhabu kwa wale abiria wanaochelewa kufika uwanja wa ndege au kushi ndwa kufika kabisa siku ya safari na wanaobadilisha tarehe za safari zao,” alisema.
Aidha, Waziri wa Zanzibar, Mwinyihaji Haji Makame, alisema inatia moyo kuona ATCL ikirejesha safari zake Zanzibar baada ya kusitisha huduma zake katika  kisiwa hicho kwa zaidi ya miaka minne, lakini aliwataka ATCL kufuata muda na kuhakikisha wanapunguza adha ya usitishaji wa safari endapo wanataka kurejesha imani miongoni mwa abiria walio wengi.
Akizungumza baada ya kupokea safari hiyo ya uzinduzi katika uwanja wa ndege wa Arusha, Mkuu wa Wilaya ya Arusha mjini, Bw. John Mongela alisema uanzaji wa safari hizo za ATCL katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Geneva ya Afrika umerejesha sifa iliyokuwa nayo ndege hiyo ya taifa kipindi cha nyuma wakati wa mikutano ya kimataifa jijini Arusha. 
“Hii ni hatua ya busara sana kwa ATCL. Jiji la Arusha alitoi tu fursa ya ndege hii kusafirisha watalii moja kwa moja kutoka Dar es Salaam kuja Arusha na kuwaunganisha kwenda Zanzibar, bali pia inawapa fursa ya kusafirisha viongozi wa kimataifa wanaosafiri mara kwa mara kuja Arusha kwa ajili ya mikutano,” alisema.
Kwa sasa, ATCL itakuwa ikitumia ndege yake aina ya Bombardier Dash – 8 yenye uwezo wa kubeba abiria 50 katika njia hiyo.

0 comments: