Thursday 14 November 2013

MTUHUMIWA WA 10 AKAMATWA NA POLISI AKIWA NA BASITOLA YA DK MVUNGI

Jeshi la Polisi mkoani Dar es Salaam limesema limemkamata mtuhumiwa John Ikondia Mayunga (56) akiwa na bastola ya marehemu Dk Mvungi aliyefariki dunia juzi.

Kamanda wa Polisi, Suleiman Kova alikaririwa akisema, “mnamo tarehe 12/11/2013 Polisi walipata taarifa kutoka kwa raia mwema kwamba kuna mtu ambaye amehusika na tukio la mauaji ya Dk Mvungi na kwamba kipindi hicho mnamo saa 12 jioni mtuhumiwa alikuwa maeneo ya mtaa wa Twiga, Jangwani akiwa anaangalia Televisheni.”

Kova akasema mtuhumiwa alitambuliwa na kukamatwa kisha kuhojiwa na Polisi na kukubali kwamba alihusika katika 
tukio hilo. Mtuhumiwa huyo  akawaongoza askari hadi nyumbani kwake Kiwalani, Migombani ambapo baada ya nyumba kupekuliwa, ilipatikana silaha ambayo ni bastola aina ya revolver namba BDN 6111 pamoja na risasi 21.

“Mtuhumiwa Mayunga alipohojiwa kuhusu umiliki wa silaha hiyo  hakuwa na kibali chochote cha umiliki wa silaha hiyo, badala yake alieleza ni kati ya vitu walivyoiba yeye na wenzake mnamo Novemba 3 mwaka huu nyumbani kwa marehemu Dk. Mvungi” alisema Kova na kuongeza: “Silaha hiyo iliyokamatwa inatambuliwa na familia ya marehemu na kwamba ilikuwa chini ya himaya yake … kabla ya tukio tumepata uthibitisho wa kumbukumbu za maandishi, pamoja na maelezo hayo kumbukumbu za nyuma zinaonyesha kuwa ni jambazi mzoefu na hivi karibuni alimaliza kifungo cha miaka saba jela kwa makosa ya ujambazi.”

Vitu vingine vilivyokutwa ni vifaa vya mlipuko/baruti aina ya Explogel yenye muundo wa sausage, Tambi 2 ambazo ni viwashio vya baruti (Detonator) na milipuko 4 ambayo imeunganishwa na tambi tayari kwa kutumia.

Kova amesema kuwa mtuhumiwa alikiri kwamba katika vitu vilivyoibwa nyumbani kwa Dk Mvungi ni pamoja na bastola hiyo.

Aidha, siku ya tukio hilo walitumia milipuko kutishia ili kufanikisha uporaji. 

 

0 comments: