KWA MUHUTASARI
XXX KLABU, MAKOCHA, WACHEZAJI WATWANGWA FAINI!
XXX FUTURE TAIFA STARS vs TAIFA STARS UWANJANI KARUME
PATA HABARI KAMILI:
Release No. 194
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Novemba 12, 2013
BODI YA LIGI YAFUNGIA VIWANJA SABA
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPL Board)
imefungia viwanja saba vilivyokuwa vikitumiwa na timu za Ligi Kuu ya
Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) hadi vitakapofanyiwa
marekebisho ili kukidhi mahitaji ya mechi za mpira wa miguu.
Uamuzi huo umefikiwa na TPL Board katika
kikao chake cha kwanza kilichofanyika juzi (Novemba 10 mwaka huu)
jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine kilipitia ripoti za
mechi za VPL na FDL katika mzunguko wa kwanza.
Viwanja vilivyofungiwa na marekebisho
yanayotakiwa kufanyika kwanza ili viruhusiwe kutumika tena ni Uwanja wa
Kaitaba mjini Bukoba (majukwaa yake yamechakaa, hivyo kuhatarisha
usalama wa watazamaji), na Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga (vyumba
vya wachezaji kubadilishia nguo (dressing rooms) havina hadhi).
Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini
Mbeya (sehemu ya kuchezea- pitch ni mbovu), Uwanja wa Kumbukumbu ya
Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha (pitch ni mbovu), Uwanja wa Ali
Hassan Mwinyi (vyumba vya kubadilishia kutumika kwa ajili ya shule ya
awali), Uwanja wa Majimaji mjini Songea (pitch ni mbovu) na Uwanja wa
Jamhuri mjini Morogoro (pitch ni mbovu).
Klabu ambazo timu zake zinatumia viwanja
hivyo zimeshaarifiwa rasmi juu ya uamuzi huo ambapo ama vinatakiwa
kuwasiliana na wamiliki wa viwanja hivyo ili wafanye marekebisho au
kutafuta viwanja vingine vya kuchezea mechi zao.
Kwa upande wa ripoti za mechi za VPL;
Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 na kupewa onyo kali kwa timu
yake ya U20 kutocheza mechi ya utangulizi walipocheza na Yanga. Pia
wanatakiwa kulipa gharama za uharibifu baada ya washabiki wao kuvunja
kioo cha basi la Yanga baada ya gharama hizo kuthibitishwa na Bodi ya
Ligi.
Pia Mbeya City imepigwa faini ya sh.
500,000 kwa washabiki wake kushambulia basi la wachezaji wa Tanzania
Prisons baada ya mechi dhidi yao, na kulipa gharama za uharibifu baada
ya kuthibitisha na Bodi ya Ligi.
Coastal Union imepigwa faini ya sh.
500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake ilipocheza na Azam kwenye
Uwanja wa Mkwakwani ambapo mwamuzi msaidizi Hassan Zani alishambuliwa
kwa mawe na kujeruhiwa mkononi na kichwa, tukio lililosababisha mchezo
kusimama kwa dakika tatu.
Beki wa Coastal Union, Hamad Khamis wa
Coastal Union amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumpiga kichwa kwa
makusudi Kipre Tchetche wa Azam. Kitendo hicho kilisababisha refa amtoe
nje kwa kadi nyekundu, hivyo atakosa mechi tatu zinazofuata za timu
yake.
Mchezaji Cosmas Lewis wa Ruvu Shooting
alifanya kitendo cha utovu wa nidhamu kwa kupiga kelele wakati mgeni
rasmi akisalimia timu na kukataa kupeana mkono na kamishna kwenye mechi
dhidi ya Rhino Rangers, hivyo amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya
sh. 500,000.
Mtunza vifaa (Kit Man) wa JKT Ruvu,
Selemani Oga aliondolewa kwenye benchi la ufundi wakati wa mechi yao
dhidi ya Mbeya City kwa kosa la kutoa lugha chafu kwa refa, hivyo suala
lake litapelekwa katika Kamati ya Maadili.
Kocha Msaidizi wa Oljoro JKT, Fikiri
Elias amepigwa faini ya sh. 500,000 na kufungiwa mechi tatu kwa
kumshambulia kwa matusi refa wakati wa mechi yao dhidi ya Ashanti
United. Naye mtunza vifaa wa timu hiyo Elas Justin amepelekwa Kamati ya
Maadili kwa kumshambulia refa kwa matusi ya nguoni.
Simba wamepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake wakati wa mechi dhidi ya Kagera Sugar.
Katika FDL, mchezaji Ally Mtoni wa Villa
Squad amepigwa faini y ash. 200,000 na kufungiwa mechi tano. Kosa lake
ni kujisaidia haja ndogo golini wakti wa mechi dhidi ya Ndanda FC
iliyochezwa mjini Mtwara.
Kamishna Paul Opiyo wa mechi ya FDL kati
ya Villa Squad na Transit Camp kwa kutokuwa makini. Katika ripoti yake
ameeleza kuwa Transit Camp ilichelewa kufika uwanjani, lakini hakusema
ilichelewa kwa muda gani.
Kocha wa Polisi Dar es Salaam, Ngelo
Nyanjabha na Meneja wa timu hiyo Mrimi Masi wamepigwa faini ya sh.
200,000 na kufungiwa mechi tatu kila mmoja kwa kuongoza kundi la
washabiki kumvamia refa wa mechi yao dhidi ya Villa Squad iliyochezwa
Dar es Salaam.
Pia Bodi ya Ligi imeagiza Polisi
waandikiwe barua ya onyo kwa vile wakati waamuzi wanapigwa walikuwepo
lakini hawakutoa msaada kwa wakati.
Kocha wa Friends Rangers, Kheri Mzozo
amepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi sita kwa kosa la
kumtukana refa na kutishia kuhamamisha washabiki waingie uwanjani
kufanya fujo kwenye mechi dhidi ya Villa Squad.
Naye Kocha msaidizi wa timu ya Transit
Camp, Haji Amiri amepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi sita
kwa kutoa lugha ya matusi kwa mwamuzi wa akida wakati wa mechi dhidi ya
Friends Rangers.
Adhabu zote zimetolewa kwa mujibu wa
kanuni. Pia Bodi ya Ligi imeahirisha kufanya uamuzi wa mechi kati ya
Stand United na Kanembwa JKT iliyochezwa Uwanja wa Kambarage ili
kukusanya taarifa zaidi. Mechi hiyo haikumalizika. Bodi ya Ligi
itakutana tena Jumapili (Novemba 17 mwaka huu).
FUTURE TAIFA STARS vs TAIFA STARS UWANJANI KARUME
Timu za Taifa za Future Taifa Stars na
Taifa Stars zinacheza kesho (Novemba 13 mwaka huu). Mechi hiyo ya
kirafiki itafanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam
kuanzia saa 10 kamili jioni.
Mechi hiyo ni maalumu kwa Benchi la
Ufundi la Taifa Stars linaloongozwa na Kim Poulsen kuangalia wachezaji
kumi kutoka Future Taifa Stars watakaoongezwa katika Taifa Stars tayari
kwa mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayochezwa Novemba 19 mwaka huu
jijini Arusha.
Watazamaji 300 tu wataruhusiwa kushuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha sh. 5,000.
Taifa Stars inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager imeingia kambini leo (Novemba 12 mwaka huu).
Miongoni mwa wachezaji wanaotarajia kuripoti ni kipa Ivo Mapunda wa Gor
Mahia
Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
0 comments:
Post a Comment