Sunday, 2 March 2014

' TUMEANZA BUNGE MAALUM LA KATIBA MPYA KWA KUSHINDWA'

 
bunge_a54c8.jpg
Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba amesema mwanzo wao umekuwa mbaya, kutokana na wengi wao kuwa na misimamo ya vyama na makundi yaliyowapeleka kwenye Bunge hilo.
Bunge hilo linaendelea kujadili na kurekebisha Rasimu ya Kanuni, zitakazotumika kuongoza mijadala ya kuboresha Rasimu ya Pili ya Katiba iliyoandikwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ili kupata Rasimu ya Mwisho ya Katiba Mpya, ambayo itakubaliwa au kukataliwa wananchi kwa kuipigia kura ya maoni.
"Siyo siri kwamba kilicho nyuma ya pazia ya ubishi uliyoibuka kwenye semina iliyolenga kurekebisha Rasimu ya Kanuni ni wengi wetu kuingia bungeni tukiwa na misimamo ya vyama au vikundi vilivyotutuma, mfumo wa kura za wazi ni wenye lengo la kudhibiti wajumbe wasikiuke maagizo waliyopewa na waliowaagiza," anaeleza Cheyo
Anasema misimamo haikutolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) peke yake bali vyama vyote vya siasa na kijamii vimejiwekea misimamo ambayo wajumbe walioingia bungeni, wameagizwa kuijengea hoja na kuisimamia, kuhakikisha inazingatiwa katika Katiba mpya ijayo.
Tofauti iliyopo kati ya CCM na vingine inatajwa na Cheyo kwamba ni kuwa na idadi kubwa ya wajumbe wa Bunge hilo, pia chama hicho kinaelezwa na mjumbe huyo kuwa ni chenye itikadi ya kuwa na misimamo na kuweka mbinu madhubuti za kuwasimamia walioagizwa kuitekeleza, kuhakikisha hawatendi kinyume.
"Tukirejesha fikra zetu nyuma, hatutakosa kumbukumbu juu ya kilichotokea enzi za Mwalimu Nyerere (Hayati Baba wa Taifa) wakati wakijadiliana na kuamua kuhamishia makao makuu ya nchi mjini Dodoma, ilifika wakati akasema, "Asiyetaka anyooshe mkono juu." Ingawa kulikuwa na wasiyotaka lakini tulibaki kimya bila kidole hata kimoja kunyooshwa," anaeleza Cheyo
Cheyo anasema ili mabishano yanayoendelea bungeni hususan kwenye hoja ya aina gani ya kura itumike; kati ya siri au ya wazi ni lazima wajumbe wote "wavue" tofauti zao, kwa kubaki na wadhifa mmoja tu wa ujumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na hivyo wawe na jukumu la kuboresha Rasimu ya Pili, ambayo itakayowasilishwa kwao na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Anahimiza wajumbe kuitikia wito wa Rais Jakaya Kikwete, unaowataka kuweka kando misimamo yao na kwamba ikiwa hilo halitatokea, misimamo ya vyama vya siasa na makundi ya kijamii itawafikisha hatua ya kutoka nje ya vikao vya Bunge pale mijadala itakapowadia na kupamba moto.
Cheyo anabainisha kuwa haafiki utaratibu wa 'wengi wape' katika kupitisha hoja na hatimaye Rasimu ya Mwisho ya Katiba, akisema; "Hili ni suala nyeti lisilohitaji kufanyiwa mzaha hata kidogo. Kupitisha hoja kwa mtindo wa wengi wape, tutapitisha kwa wingi wetu sawa lakini tunapitisha nini? Hapo ndipo patakapoibuka mabishano ambayo yatatufikisha mahala pa kutoka na aibu," anaeleza cheyo
Anaasa wajumbe wenzake kukumbuka kuwa tangu mchakato wa kutafuta Katiba Mpya nchini uanze, fedha nyingi za wananchi zimetumika na kwamba kushindwa kwao kutekeleza kwa ufanisi jukumu lililo mbele yao, kutasababishia taifa hasara ambayo bila shaka hawataweza kusamehewa na vizazi vya sasa na vijavyo.
"Tanga kuna kijiji niliona kwenye TV, wanachota maji ya kutumia kutoka kwenye kijiji kingine, wakitembea kwa miguu mwendo mrefu tena ndani ya maji. Ni bora fedha zilizotumika katika mchakato huu zingetumika kutatua kero za wananchi kama hizo. Ninachomaanisha hapa ni wajumbe tuone umuhimu wa kazi iliyo mbele yetu," anaeleza Isack Cheyo
Pamoja na kuweka kando itikadi na tofauti zao, ili kumaliza suala la kura ya siri au wazi ipigwe, Cheyo anasema ni vyema wajumbe wakafanya uamuzi kwa kuchagua baadhi ya wajumbe watakaowakilisha makundi yote yaliyomo kwenye kikao kitakachojadiliana na kuamua cha kufuata; akisema ni vigumu ndani ya kundi la watu zaidi ya 600, kufikia muafaka wa suala hilo.
Lugha za kukera bungeni
Cheyo anasema mtu yeyote anayesema ovyo tena hadharani huku akiwa mwenye umri wa utu uzima, ni ishara kwamba, hakudhibitiwa kitabia tangu akiwa katika umri mdogo; "Usipodhibitiwa kitabia ukiwa mtoto, utasema ovyo mpaka uzeeni mwako na hilo ndilo tunaloshuhudia bungeni."
Anasema ikitokea wakaamua kufuatilia historia ya malezi ya wanaotumia lugha chafu kwenye vikao vya Bunge, itathibitika kuwa anayoeleza ni kweli tupu na kwamba watu hao wanatia dosari hadhi ya taifa na kuwa mfano mbaya kwa watoto ambao wanafuatilia vipindi vya vikao vya Bunge, vinavyotangazwa moja kwa moja kwenye vituo vya televisheni na redio.
"Jana ilifika wakati nikatamani kuwaomba waeleze ikiwa wanapenda sana vijembe, waruhusu tuite vikundi vya taarabu bungeni, vitumbuize ili vitoe vijembe vilivyowekwa kitaalamu zaidi, na hapo ikumbukwe ni vikao vya kurekebisha rasimu ya kanuni, je tukianza mijadala itakuwaje? Inabidi ifike wakati tubadilike," anaeleza Isack Cheyo.
Chanzo:Mwananchi

Related Posts:

0 comments: