CHAMA Cha
Mapinduzi (CCM) kimetoa Sh milioni moja kwa familia tatu zilizofiwa na
ndugu zao katika ajali mbaya ya gari, iliyotokea Februari 27, katika
mlima wa Ipwasu, jimbo la Kalenga, Iringa Vijijini.
Kwa upande wao Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), nacho kimejipigapiga na kutoa Sh 50,000 kwa familia hizo.
Msiba huo
umetokea huku vyama hivyo vikiwa katika harakati za kuomba kura kwa
wapiga kura 85,051 wa jimbo hilo katika uchaguzi mdogo wa ubunge,
utakaofanyika Machi 16 baada ya aliyekuwa mbunge wake, Dk William Mgimwa
kufariki dunia.
Kwa
upande wake, CCM imemsimamisha Godfrey Mgimwa (32) wakati Grace Tendega
anagombea kupitia Chadema. Chama kingine kinachoshiriki uchaguzi huo ni
Chausta, kilichomsimamisha Richard Minja, ambaye hana ratiba ya kampeni
jimboni humo hadi sasa.
Katika
ajali hiyo, iliyohusisha gari la mizigo aina ya Fuso lenye namba za
usajili T250 AFJ, Hanskari Chengulla, Sabasaba Kiseve na Nyagile
Luvanda, walikufa papo hapo.
Lori hilo
mali ya Kiwanda cha Maji Afrika, lililokuwa likiendeshwa na Luvanda,
lilikuwa likipeleka maji ya chupa katika kijiji cha Tangamalenga.
Mgombea
wa CCM, Mgimwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba walikuwa
kivutio wakati mamia ya waombolezaji wakishiriki mazishi ya vijana hao.
Baada ya
miili ya marehemu kuhifadhiwa katika nyumba zake za milele, Chadema
walikuwa wa kwanza kupewa fursa ya kutoa rambirambi zao.
Katika
salamu zao, Chadema waliahidi kuchangia Sh 50,000 huku wakiahidi kuwa
pamoja na familia za waliopoteza maisha yao katika ajali hiyo.
Baada ya
kutoa rambirambi ya Sh milioni moja kwa niaba ya chama chake, Nchemba
alisema CCM imeguswa na vifo vya vijana hao, waliokuwa wakitegemewa na
familia zao pamoja na maendeleo ya Taifa.
Alisema
CCM iko pamoja na familia za marehemu katika kipindi hicho kigumu na
alimuagiza mgombea ubunge katika jimbo hilo, kuzikumbuka familia hizo
kwa kusaidia kusomesha watoto walioachwa na marehemu hao.
“Mgimwa,
haya ndio majukumu ya kisiasa, huu ni sehemu ya mzigo wako, ukishinda
uchaguzi moja ya kazi unayotakiwa kufanya ni kusaidia kusomesha watoto
wa ndugu zetu hawa waliotutoka,” alisema.
CHANZO:HABARILEO
0 comments:
Post a Comment