>>JUMAPILI: PRISONS v SIMBA, JKT RUVU v MTIBWA!
>>SIMBA FAINI USHIRIKINA, TAMBWE MATUSI!
SOMA ZAIDI:
Release No. 039
Machi 7, 2014
WANG’AMUZI VIPAJI MABORESHO STARS WAJICHIMBIA LUSHOTO
Wang’amuzi vipaji 28 wanakutana Lushoto
mkoani Tanga kwa siku saba katika mpango maalumu wa maboresho ya Taifa
Stars ambapo watatoka na orodha ya mwisho ya wachezaji waliopatikana
katika mechi za maboresho hayo zilizochezwa nchi nzima.
Katika kikao hicho, wang’amuzi hao
watapitia majina ya wachezaji walioteuliwa ikiwemo kuwaangalia tena
kwenye video kwa vile mechi zote zilirekodiwa. Wachezaji watakaoteuliwa
katika mpango huo baadaye wataingia kambini mkoani Mbeya.
Wang’amuzi vipaji ambao wanaoondoka
Machi 9 mwaka huu kwenda Lushoto ni Abdul Mingange, Boniface Pawasa,
Charles Mkwassa, Dan Korosso, Dk. Mshindo Msolla, Edward Hiza, Elly
Mzozo, Hafidh Badru, Hamimu Mawazo, John Simkoko, Jonas Tiboroha, Juma
Mgunda na Juma Mwambusi.
Kanali mstaafu Idd Kipingu, Kenny
Mwaisabula, Madaraka Bendera, Madaraka Selemani, Mbarouk Nyenga, Mohamed
Ally, Mussa Kissoky, Nicholas Mihayo, Peter Mhina, Salum Mayanga,
Salvatory Edward, Sebastian Nkoma, Sekilojo Chambua, Selemani Jabir na
Shabani Ramadhan.
Wengine ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji
ya TFF ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Kidao Wilfred,
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati
ya Vijana, Ayoub Nyenzi, Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi, Salum Madadi na
Mshauri wa Rais (Ufundi), Pelegrinius Rutayuga.
MUJUNI KUICHEZESHA AFC LEOPARDS CC
Mwamuzi Israel Mujuni ameteuliwa na
Shirikisho la Mpira wa Miguu (CAF) kuchezesha mechi ya marudiano ya
Kombe la Shirikisho (CC) Afrika kati ya wenyeji AFC Leopards ys Kenya na
SuperSport United ya Afrika Kusini.
Mujuni katika mechi hiyo itakayochezwa
kesho (Machi 8 mwaka huu) jijini Nairobi, Kenya atasaidiwa na Samuel
Mpenzu, Josepht Bulali wakati mwamuzi wa mezani atakuwa Ramadhan Ibada.
Kamishna wa mechi hiyo ni Amir Hassan
kutoka Mogadishu, Somalia. SuperSport United ilishinda mechi ya kwanza
iliyochezwa wiki mbili zilizopita mabao 2-0.
SIMBA YALIMWA FAINI KWA KUENDEKEZA VITENDO VYA KUSHIRIKINA
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB)
imeipiga faini ya jumla ya sh. milioni moja klabu ya Simba kutokana na
makosa mbalimbali ikiwemo vitendo vinavyoashiria ushirikina uwanjani.
Simba ilifanya vitendo hivyo katika
mechi yake dhidi ya Mbeya City ambapo imepigwa faini ya sh. 500,000. Pia
imepigwa faini nyingine ya sh. 500,000 kwa makocha wake Loga, Selemani
Matola na Idd Pazi kuingia uwanjani na kumzonga mwamuzi kwenye mechi
hiyo.
Naye mshambuliaji wa Simba, Amisi Tambwe
amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kushangilia bao alilofunga kwenye
mechi hiyo kwa kuonesha ishara ya matusi kwa kidole.
Mbeya City imepigwa faini ya sh. 300,000
kwa washabiki wake kuingia uwanjani kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar
iliyochezwa mjini Bukoba. Klabu za Yanga na Coastal Union zimepigwa
faini ya sh. 500,000 kila moja kwa washabiki wao kurusha chupa za maji
uwanjani wakati timu hizo zilipopambana jijini Tanga.
Kiungo wa Mtibwa Sugar, Shabani Nditi
amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumpiga mchezaji wa Simba, wakati
Salvatory Ntebe pia wa Mtibwa Sugar amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa
kumtukana refa kwenye mechi dhidi ya Mbeya City.
Pia mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Musa
Mgosi amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kosa la kupiga uwanjani kwenye
mechi dhidi ya Ashanti United ambapo vilevile atakosa mechi tatu za
ligi. Coastal Union imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa washabiki wake
kumrushia chupa za maji kipa wa Mbeya City.
Nayo JKT Ruvu imepigwa faini ya sh.
300,000 kwa kuchelewa kufika uwanjani kwenye mechi dhidi ya Simba
iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Vilevile wamiliki wa Uwanja wa Mkwakwani
jijini Tanga wameandikiwa barua ya kufanya marekebisho ya vyumba vya
wachezaji, kwa vile havina hewa ya kutosha.
Kwa upande wa Ligi Daraja la Kwanza
(FDL) klabu zilizopigwa faini kutokana na makosa mbalimbali ni Friends
Rangers (sh. 200,000), Lipuli (sh. 200,000), Majimaji (sh. 400,000),
Polisi Morogoro (sh. 400,000) na Transit Camp (sh. 200,000).
Kocha Msaidizi wa Polisi Morogoro, John
Tamba atapelekwa kwenye Kamati ya Maadili kutokana na vitendo visivyo
vya kimaadili katika mechi dhidi ya Burkina Faso.
Kiongozi wa Lipuli, Hamis Kiemba na
wachezaji Boniface Sawaka, George Enock na Green Paul watapelekwa katika
Kamati ya Nidhamu kutokana na utovu wa nidhamu waliofanya kwenye mechi
dhidi ya Kimondo.
Naye mchezaji Sangalau Nyamoka wa JKT
Kanembwa aliyelalamikiwa uhalali wake na Polisi Tabora suala lake
linapelekwa Kamati ya Nidhamu.
COASTAL, ASHANTI KUUMANA MKWAKWANI VPL
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea
kesho (Machi 8 mwaka huu) kwa mechi tatu ambapo Coastal Union itaumana
na Ashanti United kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Ruvu Shooting itaikaribisha Oljoro JKT
kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwania wakati Mbeya City
itacheza na Rhino Rangers kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini
Mbeya.
Mechi za Jumapili (Machi 9 mwaka huu) ni
Tanzania Prisons na Simba kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini
Mbeya, na JKT Ruvu na Mtibwa Sugar zitacheza Uwanja wa Azam Complex
uliopo Chamazi, Dar es Salaam.
FDL KUTIMUA VUMBI WIKIENDI
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inaendelea
wikiendi hii kwa timu za makundi yote matatu kushuka kwenye viwanja
tofauti nchini ambapo kesho (Machi 8 mwaka huu) Tessema itacheza na
Transit Camp kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Kundi B ni Burkina Faso vs Kurugenzi
(Jamhuri, Morogoro) wakati C Polisi Tabora vs Mwadui (Ali Hassan
Mwinyi), Stand United vs Pamba (Kambarage), Polisi Mara vs Kanembwa JKT
(Karume) na Polisi Dodoma vs Toto Africans (Jamhuri, Morogoro).
Mechi za Jumapili ni kundi A, African
Lyon vs Polisi Dar (Karume), Villa Squad vs Friends Rangers (Mabatini,
Pwani) na Ndanda vs Green Warriors (Nangwanda Sijaona, Mtwara). Kundi B
ni Polisi Morogoro vs Majimaji (Jamhuri, Morogoro) na Mlale JKT vs
Lipuli (Majimaji, Songea).
Boniface Wambura Mgoyo
Media and Communications Officer
Tanzania Football Federation (TFF)
0 comments:
Post a Comment