XX WATATU WAOMBEWA ITC KUCHEZA UJERUMANI
XX TANZANITE YATUA SALAMA MAPUTO
XX MECHI YA JKT RUVU, COASTAL YAINGIZA LAKI 2/-
XX KESSY KUSIMAMIA MECHI YA KOMBE LA DUNIA
PATA HABARI KAMILI:
Release No. 191
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Novemba 8, 2013
UHAI CUP KUANZA KUTIMUA VUMBI NOV 17
Michuano ya Kombe la Uhai
inayoshirikisha wachezaji wenye umri chini ya miaka 20 wa klabu za Ligi
Kuu inaanza kutimua vumbi Novemba 17 mwaka huu katika viwanja vya Karume
na Azam Complex, Dar es Salaam.
Droo ya michuano hiyo inayodhaminiwa na
Maji Uhai imefanyika leo (Novemba 8 mwaka huu) mbele ya waandishi wa
habari katika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
ambapo timu zimepangwa katika makundi matatu.
Kundi A linaundwa na timu za Azam,
Coastal Union, JKT Ruvu Stars, Mbeya City na Yanga, wakati kundi B ni
Ashanti United, Mgambo Shooting, Oljoro JKT na Ruvu Shooting. Kagera
Sugar, Mtibwa Sugar, Rhino Rangers na Tanzania Prisons ndizo zinazounda
kundi C.
Mechi za ufunguzi kundi A Novemba 17
mwaka huu ni kati ya Azam na Coastal Union (saa 2 asubuhi- Karume),
Yanga na Mbeya City (saa 8 mchana- Karume). Kundi B ni Ruvu Shooting na
Ashanti United (saa 4 asubuhi- Karume), Oljoro JKT na Simba (saa 10
jioni- Karume).
Kagera Sugar na Mtibwa Sugar (saa 2
asubuhi- Azam) na Rhino Rangers na Tanzania Prisons (saa 10 jioni- Azam)
ndizo zitakazocheza mechi za ufunguzi Novemba 17 mwaka huu katika kundi
C.
Robo fainali ya michuano hiyo itachezwa
Novemba 24 na 25 mwaka huu wakati nusu fainali itapigwa Novemba 26 na 27
mwaka huu. Mechi ya kutafuta mshindi wa tatu na ile ya fainali
zitachezwa Novemba 30 mwaka.
TANZANITE YA TUA SALAMA MAPUTO
Kikosi cha timu ya Taifa ya wanawake
chini ya miaka 20 (Tanzanite) kimewasili salama jijini Maputo, Msumbiji
tayari kwa mechi ya marudiano ya raundi ya kwanza ya Kombe la Dunia
itakayochezwa kesho (Novemba 9 mwaka huu).
Kwa mujibu wa kiongozi wa msafara wa
Tanzanite, Kidao Wilfred ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), timu hiyo chini ya Kocha
wake Rogasian Kaijage ilifanya mazoezi yake ya kwanza jana asubuhi.
Tanzanite itafanya mazoezi yake ya
mwisho leo (Novemba 8 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa wa Zimpeto ambao
ndiyo utakaotumika kwa mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10 kamili
jioni kwa saa za Msumbiji.
Nao wachezaji waliobaki kumalizia
mtihani yao ya kidato cha nne wameondoka leo saa 11 jioni kwa ndege ya
LAM wakiongozwa na naibu kiongozi wa msafara, Khadija Abdallah Nuhu
ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Soka cha Zanzibar
(ZFA).
KESSY KUSIMAMIA MECHI YA KOMBE LA DUNIA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika
(CAF) limemteua Lina Kessy kuwa kamishna wa mechi ya Kombe la Dunia
Kanda ya Afrika kwa wanawake chini ya umri wa miaka 20 kati ya Afrika
Kusini na Botswana.
Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya
kwanza itachezwa nchini Afrika Kusini, Novemba 9 mwaka huu. Waamuzi
kutoka Zambia ndiyo watakaochezesha mechi hiyo namba kumi.
Waamuzi hao wataongozwa na Glads lengwe
atakayepuliza filimbi wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Bernadette
Kwimbira kutoka Malawi, namba mbili ni Mercy Zulu na mezani atakuwepo
Sarah Ramadhani, wote wa Zambia.
Afrika Kusini ilishinda mechi ya kwanza
ugenini mabao 5-2. Mshindi wa mechi hiyo atacheza raundi ya pili na
mshindi wa mechi kati ya Tanzania na Msumbiji.
MECHI YA JKT RUVU, COASTAL YAINGIZA LAKI 2/-
Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati
ya wenyeji JKT Ruvu na Coastal Union ya Tanga iliyochezwa juzi (Novemba 6
mwaka huu) Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam imeingiza sh. 201,000.
JKT Ruvu iliibuka na ushindi wa bao 1-0
katika mechi hiyo namba 85 na kushuhudiwa na watazamaji 67 waliokata
tiketi kwa viingilio vya sh. 3,000 na 10,000.
Kila klabu ilipata mgawo wa sh. 39,010 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 30,661.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni
asilimia 15 ya uwanja sh. 19,835, tiketi sh. 38,100, gharama za mechi
sh. 11,901, Bodi ya Ligi sh. 11,901, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa
Miguu (FDF) sh. 5,950 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam
(DRFA) sh. 4,628.
Nayo mechi kati ya Ashanti United na
Simba iliyochezwa juzi Uwanja wa Taifa imeingiza sh. 24,931,000 ambapo
kila klabu ilipata mgawo wa sh. 5,333,590.
Wakati huo huo, mechi za jana (Novemba 7
mwaka huu) kati ya Yanga na Oljoro imeingiza sh. 34,902,000 kutokana na
watazamaji 6,045 ambapo kila klabu imepata sh. 7,812,477.95. Mechi ya
Azam na Mbeya City iliyochezwa Azam Complex yenyewe imeingiza sh.
15,973,000 kwa watazamaji 4,857 na kila klabu imepata sh. 3,953,162.
WATATU WAOMBEWA ITC KUCHEZA UJERUMANI
Watanzania watatu wameombewa Hati ya
Uhamisho wa Kimataifa (ITC) na Chama cha Mpira wa Miguu Ujerumani (DFB)
ili wacheze mpira wa miguu nchini humo.
Wachezaji hao ni Charles Mishetto na
David Sondo wanaombewa hati hiyo ili waweze kujiunga na timu ya SpVgg
1914 Selbitz, wakati Eric Magesa ameombewa kibali hicho ili achezee timu
ya klabu ya SC Morslingen.
Hata hivyo, katika maombi hayo DFB
haikuleza hapa nchini walikuwa wakicheza katika klabu zipi. Wachezaji
wote wameombewa hati hiyo kama wachezaji wa ridhaa.
Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment